Shirika la Habari ya Kimataifa la Ahlul Bayt (a.s) - ABNA - : Hadithi inaanzia pale ambapo Iblisi (Shetani), ambaye ni kiumbe mwenye asili ya jini (majini) - kwa maana ameumbwa kwa - maada - ya moto), alipokataa kutii amri ya Mwenyezi Mungu ya kumsujudia Adam(a.s). Alikataa na kuasi amri hiyo kwa kiburi cha wazi kabisa, kwa sababu alimwona Mwanadamu hastahili cheo hicho, na kwa hoja isiyo na msingi, alikataa kukubali uongozi wa Adam (a.s).
Matokeo yake, alijinunulia mwenyewe laana ya milele kutoka kwa Mwenyezi Mungu na akafukuzwa kutoka katika sehemu takatifu ya Mola. Hata hivyo, Iblisi hakusalimu amri (kwa sababu ya kiburi chake kuwa katika kiwango cha juu kupindukia). Kwa ujasiri wa ajabu!, alimwomba Mwenyezi Mungu ampe muda (Muhula wa Kuishi kwa muda mrefu, kwamba asimfishe haraka):
قَالَ رَبِّ فَأَنْظِرْنِي إِلَىٰ يَوْمِ يُبْعَثُونَ
Akasema: Mola wangu! Nipatie muda hadi siku ambayo watu watafufuliwa." (1)"
Shetani alimwomba Mwenyezi Mungu ampe muda hadi "Siku ya kufufuliwa kwa Wanadamu" (Yawm al-Ba'th), lakini Mwenyezi Mungu alimpa muda hadi "Siku ya muda maalumu uliofahamika" au kwa ibara nyingine: "Siku ya Wakati Maalum" (Yawm al-Waqt al-Ma'lum).
قَالَ فَإِنَّكَ مِنَ الْمُنْظَرِينَ
إِلَىٰ يَوْمِ الْوَقْتِ الْمَعْلُومِ
Hivyo basi, swali linabakia: Kwa nini Mwenyezi Mungu alimpa adui huyu katili na mharibifu wa imani muda wa kuwapotosha watoto wa Adam?
Ingawa Qur'an Tukufu haielezi wazi sababu ya kumpa Shetani Muda (Muhula); Lakini Imam wa Haki na Mnenaji wa Ukweli, Amirul Mu’minin (a.s), amefunua (amebainisha na kuweka wazi) hekima iliyojificha katika uamuzi huu wa kimungu. Katika khutba ya kwanza ya Nahj al-Balagha, anasema:
«فَأَعْطَاهُ اللَّهُ النَّظِرَةَ اسْتِحْقَاقاً لِلسُّخْطَةِ وَ اسْتِتْمَاماً لِلْبَلِیَّةِ وَإِنْجَازاً لِلْعِدَةِ»
"Mwenyezi Mungu alimpa muda Shetani, kwa sababu alistahili ghadhabu, ili kukamilisha mtihani, na kutimiza ahadi."
Hebu tuchambue kwa makini ibara hizi tatu:
"Kwa sababu ya Kustahili Ghadhabu" (استحقاقاً لِلسُّخْطَةِ)
Neno "سُخْطَة" linatokana na asili ya "sukht" likiwa na maana ya ghadhabu na kutoridhika kabisa, kinyume cha ridhaa (kuridhia).
Maana ya sehemu hii ni kwamba Mwenyezi Mungu alimpa Iblisi muda (au muhula aliouomba, lakini) si kwa rehema (kwa kumhurumia) au kuokoa (kwamba amelenga kumuokoa ili autumie muda huo kujisahihisha na kupata uongofu na kurudi katika mstari mnyoofu), bali (alimkubalia na kumpa muhula au muda mrefu wa kuishi) kwa ajili ya kufichua kiwango cha uasi na upotovu wake hadi kilele cha juu, ili awe ni mwenye kustahili laana na adhabu kabisa na kikamilifu.
- Inaweza kuulizwa swali hili: Je, ina maana Iblisi hakuwa tayari anastahili ghadhabu kwa uasi wake wa kwanza? Kwa nini apewe nafasi ya kuongeza dhambi?!.
- Jibu ni: Ndiyo, tayari alikuwa amestahili laana. Lakini (siri na falsafa ya) muda aliopatiwa ulikuwa wa kuonyesha zaidi na wazi uhalisia wake wa upotovu, ili uhalisia wake usiishie kufichuka na kuwa wazi katika ulimwengu wa roho (kwa maana: Ulimwengu wa Malakut - au Ulimwengu wa ufalme wa juu) tu, bali ufichuke pia hata kwa watu wote duniani.
Alipewa fursa kuonyesha uovu wake kwa dhahiri, na kuufikisha kutoka (hali ya) uwezekano mpaka kufikia katika hali halisi.
Katika Qur'an pia tunasoma:
وَإِنَّ عَلَيْكَ اللَّعْنَةَ إِلَىٰ يَوْمِ الدِّينِ
Na hakika laana itakuwa juu yako mpaka siku ya Kiyama." (2)"
Kwa hiyo, muda huo aliopatiwa (mpka siku ya wakati maalum) siyo neema kwa Shetani, bali ulikuwa ni hatua ya kukamilisha kesi iliyofunguliwa kwa sababu ya uasi wake.
"Kwa ajili ya Kukamilisha Mtihani" (استِتْمَاماً لِلْبَلِیَّةِ)
Neno "بَلِیَّة" linatokana na "ابتلاء" likiwa na maana ya jaribio au mtihani. "استتمام" maana yake ni kukamilisha kikamilifu.
Hivyo "استِتْمَاماً لِلْبَلِیَّةِ" maana yake ni "kukamilisha jaribio - mtihani - kikamilifu".
Hapa, Imam anaashiria mtihani ambao haukuwa wa Shetani, bali kwa Wanadamu. Mwenyezi Mungu alimpa Shetani muda ili atekeleze kikamilifu jukumu lake kama chombo cha mtihani — akawa ni nguvu ya nje (ya Mwanadamu) inayowapinga Wanadamu, iliyo sambamba na nafsi ni yenye kuamrisha maovu mno (إِنَّ النَّفْسَ لَأَمَّارَةٌ بِالسُّوءِ / Surat Yufus: Aya ya 53).
Uwepo wa kudumu (wa muda mrefu) wa Shetani na vishawishi vyake unamweka Mwanadamu katika njia ya kupanda na kukua; kwani analazimika kuchagua kwa hiari yake, kupambana na kushinda.
Kwa maneno mengine: Kama njia ya haki ingekuwa rahisi bila vikwazo vyovyote vile, basi kwa hakika haingekuwa na thamani kubwa.
"Kwa ajili ya Kutimiza Ahadi" (إِنْجَازاً لِلْعِدَةِ)
(إِنْجَاز) "Injaz" maana yake ni kutimiza au kutekeleza ahadi, na "عدة" ni ahadi yenyewe.
Hapa, inawezekana (na ihtimali hii ina nguvu zaidi kuwa) maana ya ahadi (inayokusudiwa) ikawa ni ile Ahadi ya Mwenyezi Mungu kuhusu malipo (thawabu) ya matendo, au utekelezaji (na utimizaji) wa mfumo wa Haki na Uadilifu.
Baadhi ya wafasiri, kama vile Marehemu Al-Khoei katika Minhaj al-Bara'ah (3), wanasema: Shetani kabla ya kuasi kwake, alikuwa amemwabudu Mwenyezi Mungu kwa maelfu ya miaka. Mfumo wa Haki na Uadilifu wa Mwenyezi Mungu unataka kwamba hata kiumbe mwenye uasi naye apate thawabu ya matendo yake mema ya zamani.
Kwa hiyo, Mwenyezi Mungu alimpa Shetani (Iblisi) thawabu ya matendo yake mema ya zamani kwa kumpa muda (muhula) wa kuishi (kwa muda mrefu) duniani — lakini kwa njia (na namna) ambayo haitamnufaisha (kwa lolote lile) Akhera.
Kwa maneno mengine: Muda huo (aliopewa Shetabni) ni aina ya kumlipa haki yake na kumalizana naye kabla ya Siku ya Kiyama, ili Siku hiyo abaki na adhabu tu, bila kuwa na hoja au kisingizio chochote.
Hitimisho:
Maneno haya ya nuru ya Imam Ali (a.s) yanaonyesha kwamba kumpa Shetani muda hakukuwa uamuzi wa ghafla, bali ni sehemu ya mpango mkubwa wa kiungu katika uendeshaji wa uumbaji. Mpango unaodhihirisha uadilifu wa Mwenyezi Mungu, unaoliweka jukumu la Mwanadamu kuwa waziwazi (na bayana), na unaomuanika Shetani kwa aibu na fedheha kamili.
Tanbihi na Marejeo:
-
Surah al-Hijr, Aya 36-38
-
Surah al-Hijr, Aya 35.
-
Minhaj al-Bara'ah, Al-Khoei, Juzuu ya 2.
Makala hii imeandaliwa na: Sheikh Taqee Zachalia Othman.
Your Comment