29 Aprili 2025 - 20:00
Source: Parstoday
Kremlin: Russia inaweza kutoa msaada wa kijeshi kwa Korea Kaskazini 'ikiwa italazimu'

Ikulu ya Russia, Kremlin imesema nchi hiyo inaweza kutoa msaada wa kijeshi kwa Korea Kaskazini chini ya makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mwishoni mwa mwaka jana.

Hayo yameelezwa na msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov mbele ya waandishi wa habari na kufafanua kwa kusema: "tuna makubaliano yetu wenyewe yanayofanya kazi, na kwa mujibu wa makubaliano haya, kiukweli pande husika zimejitolea kupeana msaada mkubwa ikiwa inalazimu".

Peskov amesema, kushiriki wanajeshi wa Korea Kaskazini katika juhudi za Russia za kulidhibiti tena eneo la mpakani la Kursk kulionyesha ufanisi wa makubaliano ya ushirikiano wa kimkakati yaliyotiwa saini kati ya nchi hizo mbili mnamo Novemba mwaka jana.

Msemaji huyo wa Kremlin ameongeza kuwa Russia inatarajia kuona ishara kutoka kwa Ukraine juu ya kuanzisha tena mazungumzo ya ana kwa ana lakini haijaona hatua yoyote kuhusiana na suala hilo.

Katika maelezo hayo aliyotoa mbele ya waandishi wa habari, Peskov amekanusha taarifa za kufanyika mazungumzo yoyote mapya kati ya Rais wa Russia Vladimir Putin na Rais wa Marekani Donald Trump, lakini akasema yanaweza kuafikiwa haraka ikiwa italazimu.

Kuhusiana na madai ya Ukraine kwamba ingali ipo kwenye eneo la mpakani la Russia la Kursk, Peskov amesema: "ninashauri kuwa muendelee kuzingatia maneno ya rais wetu".

Vilevile amesisitizia utayari wa Moscow wa kuanza mazungumzo na Ukraine bila ya masharti.

Siku ya Jumamosi, Mkuu wa Majeshi ya Russia Valery Gerasimov alitangaza kuwa nchi hiyo imelidhibiti tena eneo la mpakani la Kursk, huku pia akitoa shukurani kwa wanajeshi wa Korea Kaskazini walioshiriki katika harakati za kijeshi katika eneo hilo katika kilichoonekana kuwa ni uthibitisho wa kwanza rasmi wa kuhusika Pyongyang katika vita vya Russia na Ukraine, vilivyoanza Februari 2022.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha