1 Mei 2025 - 23:39
Source: Parstoday
Je, dunia itabaki kuwa mtazamaji pekee wa mauaji ya kimbari Gaza?

Ukanda wa Gaza uko katika janga kubwa la kibinadamu. Katika miezi iliyopita, kushadidi mzingiro wa utawala haramu wa Israel katika eneo hilo sambamba na mashambulizi ya mara kwa mara ya angani na nchi kavu, na vizuizi vikali vya misaada ya kibinadamu vilivvyowekwa na utawala huo wa Kizayuni vimeharibu si tu miundombinu ya msingi ya eneo hilo, bali pia vimeweka hatarini matumaini ya kuendelea kuishi kwa malaki ya raia wa Palestina.

Wakati janga la kibinadamu Gaza linazidi kuwa na sura za kutisha kila siku, Umoja wa Mataifa umetangaza onyo kali kuhusu kuporomoka kabisa kwa mfumo wa afya Gaza; kuporomoka huko kunatokana na kuzingirwa kikamilifu na wanajeshi wa Israel na kuzuia kwao kuingia kwa misaada muhimu, ikiwemo mafuta na vifaa vya matibabu.

Kinachoshuhudiwa leo na jumuiya ya kimataifa si tu janga la  kiafya; bali ni mfano wa ukiukaji wa wazi na wa mfumo wa haki za binadamu, hasa haki ya kuishi, afya na utu wa watu wa Gaza. Hii ni pamoja na ukweli kwamba licha ya uvunjaji wa sheria zote za vita za kimataifa, haki za binadamu na kanuni za msingi za kibinadamu, nchi nyingi duniani zimebaki kimya mbele ya uhalifu huu, na bado zinaendelea kuunga mkono utawala katili wa Israel.

Israel, ikipata uungaji mkono kamili wa wa Marekani, baada ya operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023, ilianzisha vita vya uharibifu mkubwa dhidi ya wakaazi wa Ukanda wa Gaza. Kwa kufunga njia zote za kuingiza dawa na chakula, kuendeleza mashambulizi ya mabomu na hata kuchoma mahema ya wakazi wa Gaza, Israel sasa inatekeleza moja ya mauaji makubwa ya kimbari katika historia.

Katika ripoti yake ya karibuni, Umoja wa Mataifa umeonya kwamba mfumo wa afya katika Ukanda wa Gaza uko karibu kuporomoka kabisa. Upatikanaji wa huduma muhimu za afya umepunguzwa sana katika eneo zima, na zaidi ya watu 150,000 wako katika hali mbaya kiafya. Hali imekuwa mbaya kiasi kwamba akiba ya mafuta, hasa petroli na dizeli, iko katika kiwango cha hatari. António Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, amesema: hali ya kibinadamu Gaza imekuwa mbaya zaidi na isiyoweza kufikirika. Kwa karibu miezi miwili mfululizo, Israel imezuia chakula, mafuta, dawa na mahitaji ya kibiashara, na kuwakosesha zaidi ya watu milioni mbili misaada muhimu.

Hapo awali, Agnes Callamard, Katibu Mkuu wa Amnesty International, pia alieleza katika utangulizi wa ripoti yao ya kila mwaka kuhusu haki za binadamu: tangu tarehe 7 Oktoba 2023, dunia imeshuhudia mauaji ya kimbari mubashara kwenye skrini zake.

Hali hii inaendelea huku utawala wa Israel ukiendelea na sera za kuzingira Gaza na kuua Wapalestina bila kujali sheria yoyote au onyo lolote. Mauaji haya hayajakumbana tu na ukimya wa washirika wa Israel, bali pia na uungaji mkono unaoendelea wa nchi za Magharibi, hasa Marekani, kwa Waziri Mkuu Netanyahu na operesheni zake za mauaji.

Je, dunia itabaki kuwa mtazamaji pekee wa mauaji ya kimbari Gaza?

Paul Magnette, mbunge wa Ubelgiji, amesema: jeshi la Israel linabomoa nyumba kutoka msingi, linaangamiza shule za Wapalestina, linaziba visima ili kuwanyima Wapalestina uwezo wa kuendelea kuishi katika ardhi yao. Linawapa silaha walowezi ili wawapige risasi Wapalestina kwa karibu. Haya si maneno ya kuelezea mgogoro tena, bali ni ushahidi wa uhalifu unaoendelea mbele ya dhamira ya ubinadamu.

Israel inaendelea na mauaji ya kimbari Gaza wakati ambapo Zane Dangor, mwakilishi wa Afrika Kusini katika siku ya pili ya kikao cha kusikiliza cha Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), alisema: mauaji ya kimbari Gaza yanaendelea mbele ya macho ya dunia. Aliitaka jumuiya ya kimataifa kuacha kuwa watazamaji wa kimya wa janga hili.

Kukabiliana na mauaji ya kimbari ya Wapalestina sasa ni mtihani kwa jumuiya ya kimataifa, ni mtihani kwa uhalali wa mashirika ya kimataifa, uhalali wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu huko The Hague; na pia ni mthihani kwa nchi zinazodai kuzingatia “mpangilio unaotegemea sheria.”

Ni wazi kuwa, dunia ikiendelea kufumbia macho au kutojali sera za Israel kuhusu Gaza, maisha ya watu wa Palestina yataendelea kuwa mateka wa siasa za kivita na ukoloni. Inaonekana wakati umefika kwa nchi kuchukua hatua, kama vile kuweka vikwazo vya silaha dhidi ya utawala katili Israel, kuitambua Palestina kama nchi huru, kuwasilisha malalamiko rasmi katika mahakama za kimataifa, na kukatisha ushirikiano na miradi ya walowezi, ili kusitisha mchakato wa uhalifu unaoendelea.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha