Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) – ABNA – baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah, Katibu Mkuu wa zamani wa Hizbullah nchini Lebanon, na kuundwa kwa serikali mpya ya Lebanon kwa ushawishi wa nchi za Magharibi na Marekani, mazingira ya ndani ya Lebanon yameelekea kwenye fitna na migogoro ya kimadhehebu kwa kuingiliwa kati na mataifa ya Kiarabu na Magharibi.
Uvunjaji wa mara kwa mara wa usitishaji vita na utawala wa Kizayuni chini ya kimya cha serikali ya Lebanon, kampeni za kuhamasisha kuondolewa silaha za Hizbullah, na kusambazwa kwa matamshi ya baadhi ya wanasiasa dhidi ya mrengo wa muqawama na Hizbullah, yote hayo yameunda hali ya sintofahamu na hatari ndani ya Lebanon.
Hivi karibuni, televisheni ya Al-Jadeed ilirusha ripoti kutoka kwenye kaburi la shahidi Sayyid Hassan Nasrallah ambayo, kwa mujibu wa mwakilishi wa mrengo wa muqawama, ni matusi kwa "Sayyid al-Shuhadaa wa Muqawama" (Bwana wa Mashahidi wa Mapambano).
Kituo cha televisheni Al-Manar kikilaani vikali ripoti hiyo – ambayo inalenga kuchochea mgawanyiko katika jamii ya Lebanon kupitia matusi kwa shahidi mkuu wa muqawama – kiliandika: “Filamu ya dakika tisa yenye uchochezi na ya kifahari iliyotangazwa chini ya jina la ‘uchunguzi wa uandishi wa habari’ kupitia Al-Jadeed, ilionekana kama tamko la kiusalama lisilo na saini ya mtayarishaji, bila chanzo cha kitaaluma na bila viwango vya msingi vya uandishi wa kitaalamu.”
Ripoti hiyo ilijaa vichwa vya habari vya kupikwa vilivyojengwa si kwa hoja, bali kwa minong’ono ya mitandaoni yenye lengo la kuchochea migawanyiko ya ndani. Wanaosimamia ripoti hizo si watafuta ukweli, bali ni watu wanaolenga kudhoofisha harakati na kuigawa jamii.
Mtu aliyekuwa akiunganisha taifa katika maisha yake, hata katika kifo chake, hatavunjwa na vipindi vya televisheni vya uchochezi. Na wale waliodumu katika mapambano wakati wa vita, hawatashindwa kwa ripoti za kulipwa wala kampeni za vyombo vya habari vilivyopangwa.
Kile kilichoonyeshwa na kituo kimoja cha televisheni cha Kilebanoni kuhusu kaburi la shahidi mashuhuri, Sayyid Hassan Nasrallah, hakikuwa ripoti ya kawaida, bali ilikuwa tamko la kisiasa dhidi ya jamii nzima, ikikashifu kile kilicho cha heshima na thamani zaidi kwao – baada ya kushindwa kwa mashambulizi ya awali ya vyombo vya habari kuathiri hadhi ya shahidi huyo.
Lakini kwa nini kabla hata damu ya Sayyid kukauka, mnadhalilisha nafasi tukufu yake na kushambulia moyo wa jamii yake? Nani aliilazimisha televisheni hiyo kuandaa ripoti hii ya kuumiza, na kucheza juu ya maumivu ya jamii nzima?
Ibrahim Mousawi, Mbunge wa Lebanon na mjumbe wa mrengo wa Uaminifu kwa Mapambano, ameelezea maoni yake kuhusu tukio hilo katika mahojiano na kituo cha Al-Manar.
Mousawi, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Mawasiliano ya Bunge, alisema kuwa tunakabiliwa na hali isiyo ya kawaida ya machafuko ya vyombo vya habari, akilielezea tukio hilo kama uhalifu kamili wa kimataifa katika kiwango cha habari na mawasiliano.
Katika mahojiano hayo, Mousawi alisema: "Uhalifu huu umetokea wakati mgumu, nyeti na wa hatima kwa taifa na watu wake. Ni shambulio la moja kwa moja dhidi ya malengo matakatifu na yenye thamani zaidi – yaani, malengo ya mashahidi."
Aliongeza kuwa: "Sayyid wa mashahidi wa umma, Shahidi mpendwa Sayyid Hassan Nasrallah, hakuwa mwakilishi wa madhehebu, chama au kundi fulani pekee, bali alikuwa mwakilishi wa watu wote huru, waadilifu na wanaopinga dhulma katika umma huu na kote duniani."
Mousawi alisisitiza kwamba televisheni ya Al-Jadeed, ambayo ilirusha ripoti hiyo ya uongo, iliyotungwa na kupotosha, ina wajibu wa kuomba msamaha rasmi na kukiri kosa hilo kubwa. Alisema: "Tunawauliza, mlikuwa mkilenga nini kwa kueneza ripoti hii? Kwa nini mmeichapisha sasa, na ni nani aliyeihamasisha?"
Mousawi alisisitiza kuwa: "Tunajivunia uhuru wa vyombo vya habari nchini Lebanon, lakini uhuru huu ni wa kuwajibika na unapaswa kuzingatia viwango vya kimaadili na kitaifa." Hata hivyo, aliongeza kuwa kile tunachokishuhudia sasa ni hali ya vyombo vya habari vilivyo huru bila mipaka yoyote ya maadili – hali inayosababisha kuchanganyikiwa, mifarakano na machafuko yasiyo na ulazima, ambayo yanaweza kusababisha matokeo mabaya. "Hili ni onyo la mapema – tahadhari! Hivi sivyo inavyopaswa kuendeshwa. Chombo cha habari cha kitaaluma na chenye kuwajibika hakiwezi kujiendesha kwa njia hii."
Mbunge huyo wa Lebanon pia alieleza kuwa hivi leo, kuna mwenendo ambapo baadhi ya vyama vya siasa hulipia nafasi kwenye vyombo vya habari kwa nia ya kutangaza ujumbe wa uchochezi, chuki, vurugu na utovu wa maadili, bila kuwajibika.
Akaongeza: "Jenerali Joseph Aoun, Rais wa Jamhuri, na Bwana Nawaf Salam, Waziri Mkuu – wao kwa sasa ndio viongozi wa mamlaka kuu. Waziri wa Habari na Baraza la Taifa la Vyombo vya Habari pia wana wajibu kamili wa kudhibiti maudhui haya ya vyombo vya habari."
Aliendelea kwa kusema: "Vyombo vya habari haviwezi kuwa jukwaa la kuchochea fitna. Hili halikubaliki hata kidogo, na tunalikemea vikali. Kitendo hiki kinaweza kudhoofisha hali ya utulivu wa kitaifa kwa kiwango kikubwa."
Mousawi alisisitiza kuwa: "Hatukubali kamwe kudhalilishwa au kuingiliwa kwa mara kwa mara kwa mambo yetu matakatifu na ya thamani kubwa zaidi – mashahidi wetu, waliotoa maisha yao kwa ajili ya taifa hili, heshima yake, na utu wetu. Hatutakubali yeyote aendelee kuwavunjia heshima."
Katika hitimisho, alisema: "Mamlaka ya mahakama inapaswa kuingilia kati haraka. Ikiwa hali hii ya machafuko itaendelea, hatuwezi kamwe kuwa na utulivu nchini. Pia hakutakuwepo mwanzo wowote wa kweli wa ujenzi mpya wa taifa katika awamu hii mpya."
Wananchi wanaounga mkono mapambano ya Hizbullah wanaendelea kwa njia ya Sayyid
Licha ya majaribio ya utawala wa Kizayuni kuangamiza Hizbullah kwa kuwaua makamanda wake na Katibu Mkuu wake – na kisha kuweka serikali mpya kwa msaada wa nchi za Magharibi ili kugeuza Lebanon kuwa taifa linalofuata sera za Marekani na Ulaya – adui huyo ameshindwa kuelewa mazingira ya kijamii yanayozunguka Hizbullah.
Wananchi wa Lebanon wanaounga mkono Hizbullah, hata baada ya kuuawa kwa Sayyid wa Mapambano, bado wamesimama imara licha ya maumivu makubwa, kupoteza nyumba zao, kazi zao, viungo vya miili yao, na familia zao. Lakini kwa kutoa damu zao katika njia ya mapambano, wamekuwa na nguvu zaidi. Hakuna kampeni za vyombo vya habari vya ndani vilivyo dhidi yao au mashinikizo ya kisiasa ya kigeni zitakazowazuia kufuata njia ya Sayyid wa Mapambano.
Your Comment