5 Mei 2025 - 23:28
Source: Parstoday
Yemen yatangaza mzingiro kamili wa anga dhidi ya Israel, itaendelea kulenga viwanja vya ndege

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetangaza kuwa vitaweka mzingiro kamili wa anga dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kuendelea kuvilenga mara kwa mara viwanja vya ndege vya utawala huo haramu.

Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimeeleza katika taarifa kwamba vitalenga, hasa uwanja wa ndege wa Ben Gurion ulioko mjini Tel Aviv.

Taarifa ya vikosi hivyo iliyotolewa Jumapili usiku imesema: "tunayasisitiza mashirika yote ya kimataifa ya ndege yazingatie yale yaliyoelezwa ndani ya taarifa hii kuanzia wakati wa kutangazwa na kuchapishwa taarifa yake, na kufuta safari zao zote za ndege zinazoelekea viwanja vya ndege vya adui mtenda jinai, ili kulinda usalama wa ndege zao na abiria wao."

Taarifa hiyo imeendelea kueleza: "Yemen azizi, iliyo huru na inayojitawala, haitakubali kuendelea uchokozi ambao adui anajaribu kuufanya kuzilenga nchi za Kiarabu kama vile Lebanon na Syria, na inasisitiza kuwa taifa hili halitakhofu makabiliano na halitakuwa tayari kusalimu amri na wala halitakubali kudhalilishwa".

Tangu Machi 15, serikali ya Rais wa Marekani Donald Trump imekuwa kila siku ikifanya mashambulizi ya anga dhidi ya Yemen na kudai kuwa imeshalenga zaidi ya maeneo 1,000 ndani ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Mashambulio hayo yanalenga kusitisha mashambulizi ya kijeshi ya Yemen dhidi ya meli za utawala wa Kizayuni wa Israel na zinazoelekea kwenye bandari za utawala huo ghasibu kupitia Bahari Nyekundu; na vilevile yanadaiwa kufanya ili kuzuia operesheni za kijeshi za Yemen zinazolenga maeneo ya ndani kabisa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yaliyopachikwa jina bandia la Israel.

Siku ya Jumamosi, Vikosi vya Ulinzia vya Yemen vilitangaza kuwa vilifanya shambulio la nne la makombora ndani ya saa 24 dhidi ya ngome za Israel na kusababisha ving'ora vya hatari ya mashambulio ya anga kupigwa katika maeneo mengi wanayoishi Wazayuni.

Msemaji wa Jeshi la Yemen, Brigedia Jenerali Yahya Saree, alithibitisha katika taarifa kwamba Sana'a ililenga eneo la jeshi la utawala wa Kizayuni kusini mwa Tel Aviv katika operesheni ya kulipiza kisasi mapema Jumamosi asubuhi.

Tangu utawala wa Kizayuni ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Ghaza, Vikosi vya Ulinzi vya Yemen vimetekeleza operesheni nyingi za kijeshi dhidi ya ngome za utawala wa Kizayuni na dhidi ya meli zake na zinazoelekea kwenye bandari zake katika Bahari Nyekundu ili kuonyesha uungaji mkono kwa Wapalestina madhulumu wa Ghaza.../

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha