6 Mei 2025 - 18:17
Onyo Kuhusu Mradi wa "Kuisahau Palestina" – Njama ya Kimataifa kwa Ushirikiano wa Viongozi wa Kiarabu

Kiongozi wa Harakati ya Kuamsha Ummah wa al-Mustafa: Kusahau Kadhia ya Palestina ni Njama Hatari na Usaliti Usiosameheka. Kiongozi wa Harakati ya Kuamsha Ummah wa Mustafa, katika hotuba yake ya hivi karibuni mjini Lahore, amekosoa vikali ukimya wa ulimwengu wa Kiislamu mbele ya uhalifu wa utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Palestina. Amesema kuwa kusahaulika kwa suala la Palestina ni njama hatari na usaliti usiosameheka, na akasisitiza kwamba ukimya huu – kuanzia vyombo vya habari hadi baadhi ya Serikali za Kiarabu – ni sehemu ya mradi wa kufuta kwa taratibu Palestina kutoka kwenye kumbukumbu ya Ummah wa Kiislamu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Ahlul-Bayt (a.s) – ABNA – Hujjatul Islam Sayyid Jawad Naqvi, Kiongozi wa Harakati ya Kuamsha Ummah wa al-Mustafa nchini Pakistan, katika hotuba yake ameeleza kuwa:

“Katika zama za sasa, nguvu ya vyombo vya habari, michezo ya kisiasa na mbinu za kutengeneza simulizi za kijamii, zimekuwa silaha hatari na zenye nguvu kwa ajili ya kudhibiti upeo wa ufahamu wa Mwanadamu.”

Ameonya kuwa kwa kutumia silaha hizo, njama hatari na iliyoratibiwa vema inatekelezwa kwa jina la “kusahaulika kwa Palestina.” Njama hii, amesema, si ya Wazayuni na Marekani pekee, bali baadhi ya watawala wa Kiarabu pia wamekuwa sehemu yake na sasa ni walinzi wa maslahi ya utawala wa Kizayuni.

Naqvi amesema:

“Rasilimali za kifedha za Waarabu zinatumika katika miradi ya mabilioni ya dola – lakini si kwa ajili ya Gaza, wala kwa ajili ya Msikiti wa Al-Aqsa, au kwa ajili ya mayatima na wajane wa Palestina – bali kwa lengo la kufuta jina la Palestina kutoka kwenye kurasa za historia.”
“Mpango wao ni kuisahaulisha Palestina kwanza, kisha kuifanya kuwa bidhaa ya kuuza. Wanataka kuiondoa kutoka kwenye kumbukumbu, ili baadae waiuze kisiasa.”

Ameeleza kuwa huu si uvumi, bali ni ukweli unaoshuhudiwa kwa macho, huku baadhi ya serikali za Kiarabu zikianzisha uhusiano wa wazi na Israel, kuwageuka Wapalestina kwa hila, na kuiacha Al-Aqsa mikononi mwa wavamizi.

Hata hivyo, amesema historia imethibitisha kuwa njama hizo zimevunjwa na mhimili wa muqawama, unaojumuisha Hamas, Hizbullah, Ansarullah, na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ameongeza:

“Mhimili huu umeonesha kwa ulimwengu kuwa kusahaulika kwa Palestina haiwezekani, na kuuzwa kwake hakutakubalika. Kila mara tangazo la kusitisha mapigano linapotolewa, huambatana na mashambulizi mapya nyuma ya pazia, huku vyombo vya habari vikinyamaza, wachambuzi wakizungumzia mada potofu, na fikra za umma zikielekezwa mbali na Gaza.”

Sayyid Naqvi pia amesema:

“Gaza bado inachomwa na moto, Al-Aqsa bado imevamiwa, watoto wa Palestina bado wanazikwa bila sanda, na mashambulizi ya mabomu bado yanaendelea – lakini sisi tumenyamaza. Wabunge wetu hata hawalitaji jina la Palestina.”

Katika hitimisho lake amesema:

“Kuisahau Palestina ni uhalifu. Kupuuza majeraha ya Gaza ni uhalifu. Kugeuka kutoka kwa Al-Aqsa ni uhalifu. Na ikiwa uhalifu huu unafanywa na mtu wa kawaida, huenda ukasameheka; lakini ukifanywa na mwanachuoni wa dini, mtawala, mwandishi wa habari, msomi, profesa, mfanyakazi wa serikali au mwanasiasa – basi huo ni usaliti usiosameheka.”

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha