Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA-Sheikh Abdul Ghani Khatibu, ametoa hotuba fupi ya mawaidha juu ya mada isemayo: "Maisha bila malengo ni maisha yasokuwa na maana."
Ujumbe wake naukuu hapa chini kama ifuatavyo:
Mawaidha Mafupi: Maisha Bila Malengo
Bismillahir Rahmanir Rahim
Sifa zote ni za Allah, Mola wa ulimwengu wote. Rehema na amani zimshukie Mtume wetu Muhammad (SAWW), na familia yake Watoharifu, Maswahaba wake wema, na wote wanaomfuata kwa wema hadi Siku ya Kiyama.
Ndugu zangu katika Imani, Leo ningependa tukumbushane ujumbe mfupi lakini wenye uzito mkubwa:
"Maisha bila malengo ni maisha yasokuwa na maana."
Kauli hii inatufundisha kuwa kila mmoja wetu anatakiwa aishi kwa malengo, kwa sababu malengo huleta mwelekeo, huleta msukumo, na huleta maana ya kweli ya maisha.
Tazama Qur'an Tukufu, Allah anatuambia:
"Na Sema: Hakika Swala yangu, na ibada zangu, na uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allah, Mola wa walimwengu." (Surah Al-An'aam 6:162)
Aya hii inatufundisha kuwa hata maisha yetu yanapaswa kuwa na lengo kuu – kumridhisha Allah. Lakini ndani ya hilo, tumepewa nafasi ya kuweka malengo mengine ya kidunia: elimu, kazi, familia, kusaidia jamii, kujenga tabia njema n.k.
Ndugu zangu,
Mtu asiye na malengo huwa hana mpangilio, haoni thamani ya muda, na mara nyingi hujikuta akipoteza maisha kwenye mambo yasiyo na tija. Lakini mwenye malengo huamka kila siku akijua anachokitafuta, huwa na subira na bidii, na hatimaye maisha yake huwa na baraka na mafanikio.
Mtume (SAWW) amesema:
"Hakika Allah anapenda anapofanya mmoja wenu kazi, aifanye kwa ufanisi." (Al-Bayhaqi)
Hili lina maana kuwa hata katika kazi au malengo yetu ya kila siku, tunapaswa kuwa na nia, na tuifanye kwa ubora – kwa sababu ndio maisha yenye maana.
Hitimisho:
Leo, kila mmoja wetu na ajiulize: Ninaishi kwa malengo au ninaishi kwa mazoea?!
Je, nina lengo la kidini, kielimu, kifamilia, au kijamii ambalo nalifanyia kazi kwa bidii?!
Tukumbuke, maisha haya ni safari. Safari bila ramani hupotea. Weka malengo yako, yashike kwa mikono miwili, na muombe Allah akukadirie kheri na mafanikio ndani yake.
Wassalamu Alaikum Warahmatullah.
Mwisho wa kunukuu.
Your Comment