Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sala ya Ijumaa tarehe [23-05-2025] katika Masjidul Ghadir, Kigogo Post, Dar-es-Salaam, imeswaliwa kwa kuongozwa na Samahat Sheikh Hemed Jalala.
Katika khutba yake ya leo, Maulana Sheikh alizungumza juu ya "Malezi ya Kidini na Kiroho kwa Watoto kama msingi wa ujenzi wa familia bora."
Sheikh Hemed Jalala alisisitiza umuhimu wa malezi bora ya watoto kwa kufuata misingi thabiti ya Kiislamu. Alibainisha kuwa familia ni msingi wa jamii, na hivyo malezi ya mtoto yanapaswa kuakisi maadili na mafundisho ya dini.
Aidha, alikumbusha jamii kuenzi na kuendeleza mila na desturi nzuri ambazo zimekuwa nguzo ya maadili mema.
Alieleza kuwa mila kama mtoto kumheshimu mkubwa, kusaidia wazee, na kutokuwa na tabia ya kuongea mbele ya watu wazima bila ruhusa, ni sehemu muhimu ya malezi ya kiroho na kijamii. Alitoa mfano wa kihistoria wa namna Imam Hussein (as) alivyokuwa hahutubii / hazungumzi mbele ya kaka yake Imam Hassan (as) bila idhini, akionyesha heshima na nidhamu ya hali ya juu.
Sheikh Jalala alihitimisha kwa kuhimiza jamii kurejea katika maadili yetu mema, desturi nzuri, na kuhakikisha watoto wetu wanalelewa katika msingi wa utamaduni wetu wa Kiislamu unaojenga nidhamu, heshima, na maadili mema.
Your Comment