28 Mei 2025 - 20:16
Source: Parstoday
Sababu za kuimarika uhusiano wa Iran na Oman

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekutana na Sultan Haitham bin Tariq wa Oman mjini Muscat na kujadiliana naye njia za kuimarisha uhusiano wa pande mbili.

Rais Masoud Pezeshkian, aliwasili Muscat, mji mkuu wa Oman, Jumanne, Mei 27 kwa ajili ya kubadilishana mawazo na Sultan wa Oman kuhusu masuala mbalimbali yakiwemo ya kuimarisha mahusiano na jirani huyo wa kusini mwa Iran na vilevile diplomasia ya eneo ya Tehran.

Katika kikao na Sultan Haitham bin Tariq wa Oman, Rais Pezeshkian amesisitiza utayarifu wa Iran wa kupanua ushirikiano katika nyuga zote na kusisitiza kuwa: "Tuna uwezo ambao tunaweza kuutumia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya kila mmoja wetu na mataifa mengine katika eneo. Katika hali kama hiyo, hakuna serikali ya kigeni itakayoweza kuyatishia mataifa ya Kiislamu."

Katika mkutano huo, Pezeshkian amesisitiza haja ya kuwezesha mabadilishano ya kiuchumi na kibiashara na kupanua ushirikiano kati ya nchi hizi mbili katika nyanja za ulinzi na usalama. Rais wa Iran ametathmini nafasi ya Oman katika siasa za nje za Iran kuwa ya kistratijia na kusema: "Iran ina imani kamili na Oman. Uaminifu huu unaongeza majukumu ya pande mbili kwa ajili ya kuimarisha zaidi mahusiano na kufuatilia maelewano yaliyofikiwa."

Sultani wa Oman pia amesema katika kikao hicho: "Iwapo njia ya shughuli za wafanyabiashara itafunguliwa, tutashuhudia uhusiano kati ya nchi hizi mbili ukiimarika pakubwa. Uhusiano kati ya bandari za Irani na Oman unapaswa kuendelezwa, na uwezo wa reli ya kaskazini-kusini wa Iran pia ni muhimu sana kwa Oman katika mtazamo wa kibiashara."

Sultani wa Oman ameendelea kusema: "Kunapaswa kuwepo uungaji mkono mkubwa zaidi wa ushirikiano katika sekta ya nishati kati ya nchi mbili, na tunakaribisha ushirikiano wowote na Iran hususan katika nyanja za kijeshi na maslahi ya pamoja."

Sababu za kuimarika uhusiano wa Iran na Oman

Haitham bin Tariq sambamba na kuthamini misimamo ya msingi na imara ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kuwatetea wananchi wa Palestina amesema: "Kusimama kidete kwa ajili ya haki za watu wa Palestina na kuwatetea raia wanaodhulumiwa ni jambo la thamani na la kupongezwa na Oman."

Wakati wa ziara rasmi ya Rais Pezeshkian nchini Oman, hati 18 za ushirikiano pia zimetiwa saini kati ya maafisa wa ngazi za juu wa nchi mbili.  Nyaraka hizi zilitiwa saini kati ya maafisa wa Iran na Oman kwa lengo la kurasimisha ushirikiano wa pande mbili na kupanua mahusiano katika nyanja za kisheria, kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni, kielimu, kiafya, kiulinzi, vyombo vya habari, teknolojia, nishati na madini.

Oman inapakana na Bahari ya Arabia upande wa mashariki na Bahari ya Oman upande wa kaskazini. Nchi hii inapakana na Yemen upande wa kusini na Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu upande wa magharibi. Oman pia ina mpaka wa baharini na Iran.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Oman zinatilia maanani kupanua uhusiano wao kwa sababu za kistratijia, kiuchumi na kiusalama. Oman iko karibu na Lango-Bahari la Hormuz, na Iran pia ni moja ya nchi muhimu katika eneo hili. Mashirikiano kati ya nchi mbili hizi unaweza kusaidia pakubwa katika kuleta utulivu katika Lango-Bahari la Hormuz, suala ambalo lina umuhimu mkubwa katika biashara ya mafuta duniani.

Iran, kutokana na akiba yake kubwa ya nishati, ikiwa ni pamoja na gesi, inaweza kuwa muuzaji mkubwa wa nishati kwa Oman. Iran inawekeza katika masoko mapya ya mauzo ya gesi nje ya nchi, na Oman inakaribisha ushirikiano na Iran katika suala hili, ikizingatiwa mahitaji yake ya ndani katika sekta ya nishati. Kiwango cha mabadilishano ya kibiashara kati ya Iran na Oman kimekuwa kikiongezeka mara kwa mara katika miaka ya hivi karibuni, ikijumuisha mauzo ya nje ya bidhaa za kilimo na viwanda.

Bandari ya Chabahar katika mkoa wa Sistan na Baluchestan nchini Iran pia itakuwa fursa kwa sekta binafsi ya Oman kuwepo na kuwekeza katika eneo hili, ambalo linaweza kuwa kituo muhimu cha mahusiano ya Oman na Asia ya Kati na vile vile Afghanistan. Oman pia ina nafasi ya upatanishi katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Iran na Marekani.

Uhusiano wa Iran na Oman daima umesimama juu ya msingi wa kuheshimiana na maslahi ya pande mbili katika miongo ya hivi karibuni, licha ya jitihada za Marekani za kuchochea chuki dhidi ya Iran katika eneo. Viongozi wa Oman wanaamini kuwa uhusiano wa karibu na Iran unatokana na uhalisia wa mambo na wanaichukulia Iran kuwa jirani mkubwa.

Bila shaka safari ya Pezeshkian mjini Muscat imekuwa na lengo la kuendeleza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni wa Iran na nchi jirani. Asili chanya ya kihistoria ya uhusiano wa Tehran na Muscat inaweka wazi msingi wa kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika miaka ijayo.

Your Comment

You are replying to: .
captcha