15 Juni 2025 - 13:21
Source: Parstoday
Israel yaendelea kukabiliwa na mvua ya makombora ya Iran; mkuu wake wa ujasusi ajiuzulu

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) usiku wa kuamkia leo limetekeleza wimbi jipya la mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya utawala wa Kizayuni, kufuatia awamu ya kwanza ya operesheni ya kulipiza kisasi ya "Ahadi ya Kweli III" Ijumaa usiku.

Wimbi hilo jipya la mashambulizi lilianza saa tano na nusu usiku wa kuamkia leo Jumapili kwa saa za hapa nchini Iran. Operesheni hiyo ya kulipiza kisasi isiyo na kifani inafanywa chini ya kaulimbiu "Ya Ali ibn Abi Talib," kwa mnasaba wa maadhimisho ya sikukuu ya Idd ya Ghadir.

Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu limesema katika taarifa kwa vyombo vya habari kwamba, mashambulizi hayo ni sehemu ya "Operesheni ya Ahadi ya Kweli III" na yalihusisha kuvurumishwa kwa makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea shabaha za Israel.

Ving'ora vya tahadhari vilisikika kote Israel usiku wa jana, huku Waisraeli wakishauriwa kukimbilia kwenye mahandaki kujikinga na mabomu katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu.

Israel yaendelea kukabiliwa na mvua ya makombora ya Iran; mkuu wake wa ujasusi ajiuzulu

Jeshi la Yemen limevurumisha makombora na kupiga Tel Aviv

Ripoti zinasema kiwanda cha kusafisha mafuta cha Haifa na vituo vya gridi za umeme zilipigwa kwa mafanikio na makombora ya Iran. 

Karibu saa mbili baadaye, SEPAH ilisema katika taarifa mpya kwa vyombo vya habari kwamba, vituo vinavyozalisha mafuta kwa ajili ya ndege za kivita za Israel na miundombinu mingine ya nishati imeathirika.

Duru za awali za mashambulizi ya Iran zilisababisha uharibifu mkubwa katika miji ya Tel Aviv na Jerusalem (Quds) na viunga vyake.

Brigedia Jenerali Ahmad Vahidi, Mshauri Mkuu wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), alisema mapema jana kuwa, duru ya kwanza ya Operesheni ya Ahadi ya Kweli III imetekelezwa kwa mafanikio makubwa na kikosi cha anga cha IRGC, na kwamba kwa akali shabaha 150 zimepigwa wakati wa operesheni ya kulipiza kisasi ya Jamhuri ya Kiislamu dhidi ya utawala haramu wa Israel.

Wakati huo huo, hapa mjini Tehran, utawala wa Israel ulipiga ghala la mafuta katika kitongoji cha magharibi mwa jiji na kusababisha moto mkubwa.

Wizara ya Mafuta ya Iran bila kutoa maelezo zaidi imetangaza kuwa, hifadhi nyingine ya mafuta pia ililengwa na hujuma ya Israel kusini mwa Iran.

Israel yaendelea kukabiliwa na mvua ya makombora ya Iran; mkuu wake wa ujasusi ajiuzulu

Ronen Bar, Mkuu wa taasisi ya kijasusi ya Israel aliyejiuzulu

Huku hayo yakijiri, Ronen Bar, Mkuu wa taasisi ya kijasusi ya utawala haramu wa Israel ya 'Shin Bet' amejiuzulu kutokana na operesheni kubwa ya kijeshi ya Iran ya kulipiza kisasi dhidi ya utawala wa Kizayuni.

Arutz Sheva, mtandao wa vyombo vya habari wa Israel, uliripoti hayo katika taarifa iliyotolewa mapema leo Jumapili na kueleza kuwa, kujiuzulu kwa Bar kumekuja miezi kadhaa baada ya kuwaonya maafisa wa utawala huo kuhusu Jamhuri ya Kiislamu "kujipenyeza" kwa kina katika masuala ya kiintelijensia ya Israel.

Your Comment

You are replying to: .
captcha