15 Juni 2025 - 13:24
Source: Parstoday
Operesheni ya Iran dhidi ya Israel itaendelea kadiri itakavyolazimu

Operesheni ya kulipiza kisasi ya Ahadi ya Kweli III inayotekelezwa na Iran dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel itaendelea kadiri inavyohitajika. Haya yamesemwa na Mshauri Mkuu wa Kijeshi wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Akizungumza na Televisheni ya taifa Ijumaa usiku, Brigedia Jenerali Ahmadi Vahidi, ambaye pia ni mshauri mkuu wa Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu IRGC, amesema Operesheni ya Ahadi ya Kweli III imepiga shabaha kadhaa za Israel katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo ghasibu.

Kambi za ndege za Nevatim na Ovda, ambamo kuna kituo cha kamandi na udhibiti cha utawala wa Israel pamoja na kituo cha vita vya kielektroniki, zimekuwa zikilengwa katika mashambulizi ya Iran.  Brigedia Jenerali Vahidi amebainisha hayo na kuongeza kuwa vituo hivyo viwili vimetumika kama sehemu ya kuendeshea na kuongoza uvamizi dhidi ya Iran.

Maeneo mengine yaliyopigwa na jeshi la IRGC ni pamoja na kambi ya anga ya Tel Nof karibu na Tel Aviv, Wizara ya Vita ya utawala wa Kizayuni pamoja na vituo vya viwanda vya kijeshi vya Tel Aviv.

Brigedia Jenerali Vahidi amesema kwamba makombora ya Iran yaliyorushwa dhidi ya utawala ghasibu wa Israel kupitia operesheni ya Ahadi ya Kweli III yalielekezwa dhidi ya jumla ya shabaha zaidi ya 150, ambazo zililengwa katika hatua kadhaa.

Jenerali huyo amesema utawala wa Israel ulifanya makosa makubwa kwa kuishambulia Iran, akionya kwamba Wazayuni wanapaswa kujitayarisha kwa ajili ya matokeo yake machungu.

Wakati wa opereshen hiyo, mamia ya makombora yalirushwa na Iran Ijumaa jioni na kuweza kuvuka kwa mafanikio mfumo wa ulinzi wa anga wenye matabaka kadhaa wa Wazayuni.

Operesheni ya Ahadi ya Kweli III imetekelezwa na majeshi ya Iran baada ya utawala haramu wa Israel kushambulia maeneo kadhaa ya makazi katika mji mkuu Tehran na maeneo mengine katika mikao ya Iran mapema Juni 13.

Operesheni ya Iran dhidi ya Israel itaendelea kadiri itakavyolazimu

Mohammad Hossein Baqeri, Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Hossein Salami, Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Meja Jenerali Gholam Ali Rashid, Kamanda wa Makao Makuu ya Khatam al-Anbia ya Iran, Meja Jenerali Amir Ali Hajizadeh, Kamanda wa Kikosi cha Wanaanga wa IRGC na wanasayansi wa nyuklia wasiopungua sita waliuawa katika mashambulio hayo ya kichokozi yaliyofanywa na utawala huo dhidi ya Iran.

Ayatullah Seyyed Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameuonya utawala wa Kizayuni kwamba, utapata adhabu kali kutokana na uchokozi huo na kuongeza: "Kwa jinai hiyo, utawala wa Kizayuni umejiandalia hatima chungu na ya kuumiza ambayo bila shaka itaufika tu."

Wakati huo huo, Esmaeil Baghaei, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa mazungumzo na Marekani kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran "hayana maana tena" kufuatia mashambulizi hayo ya Israel ambayo yamefanyika kwa uungaji mkono na ushirikiano wa moja kwa moja wa nchi hiyo na watawala wa Tel Aviv. Ameituhumu Washington kwa kuunga mkono uchokozi huo.

Amesema Marekani imefanya mambo kwa namna ambayo inafanya mazungumzo kutokuwa na maana kabisa. Amesema: "Huwezi kudai kufanya mazungumzo na wakati huo huo kugawa kazi kwa kuruhusu utawala wa Kizayuni wa Israel kulenga maeneo ya Iran." Baghaei amesema utawala wa Israel "ulifanikiwa kuathiri" mchakato wa kidiplomasia na kwamba haungeweza kufanya mashambulio hayo ya kichokozi bila ya idhini ya Washington.

Duru ya sita ya mazungumzo ya nyuklia yasiyo ya moja kwa moja kati ya Marekani na Iran yalipangwa kufanyika kesho Jumapili mjini Muscat, Oman lakini sasa haifahamiki vizuri iwapo yatafanyika au la kufuatia mashambulizi hayo ya Israel.

Rais Donald Trump wa Marekani ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba yeye na timu yake walijua kwamba mashambulizi ya Israel yanakuja lakini kwamba bado waliona kuwepo fursa ya kufikia mapatano na Tehran.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha