7 Julai 2025 - 23:12
Source: Parstoday
Hamas yakaribisha mwito wa BRICS wa kuondoka vikosi vya Israel huko Palestina

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imekaribisha kwa mikono miwili wito wa kundi la nchi zinazoinukia kiuchumi BRICS kwa utawala haramu wa Israel, wa kukomesha vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza, na kuondokaa kikamilifu katika eneo hilo la pwani lililozingirwa, na ardhi zote za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Harakati ya hiyo ya apambano ya Wapalestina yenye makao yake huko Gaza imesema hayo katika taarifa yake leo Jumatatu, ikiwa ni siku ya mwisho ya mkutano wa kilele wa BRICS mjini Rio de Janeiro nchini Brazil, ambao ulitangaza matakwa hayo kama sehemu ya taarifa yake ya mwisho.

"Tunakaribisha taarifa ya mwisho ya mkutano wa kilele wa BRICS na wito wake wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, na kuondolewa kwa vikosi vya Israel," vuguvugu hilo la Muqawama limesema.

Takriban Wapalestina 57,418, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama wa Wazayuni tokea Oktoba 7 mwaka 2023, hujuma ambazo Tel Avivi ilianzisha kujibu operesheni ya kihistoria ya wanamuqawama iliyofuata miongo kadhaa ya uvamizi na ukatili wa Tel Aviv.

Hamas imelipongeza kundi la BRICS kwa kukemea ukiukwaji mbalimbali wa sheria za kimataifa unaofanywa na utawala huo ghasibu, ikiwa ni pamoja na kushadidisha kidhalimu mzingiro wake dhidi ya Gaza.

Aidha Rais Luiz Inacio Lula da Silva wa Brazil amesema dunia lazima ichukue hatua kukomesha kile alichokitaja kama "mauaji ya kimbari" yanayofanywa Israel huko Gaza.

Lula aliyasema hayo jana katika hotuba ya ufunguzi wa kikao cha viongozi  kutoka mataifa 11 yanayoibuka kiuchumi ya kundi la BRICS waliokutana mjini Rio de Janeiro Brazil. Vile vile amesema, kuitumia njaa kama silaha ya vita hakukubaliki hata kidogo na kwamba suluhu pekee ni kwa Israel kuachana na ardhi inazozikalia kwa mabavu na kuanzishwa taifa la Palestina ndani ya mipaka ya mwaka 1967.

Your Comment

You are replying to: .
captcha