9 Desemba 2025 - 22:22
Kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania - Sheikh Dkt.Alhad Mussa Salum katika Kumbukizi ya  Miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika

Tanganyika ilipata Uhuru kwa njia ya Amani; na sisi leo hii tunalo jukumu la kuuimarisha na kuurithisha kwa vizazi vijavyo. Kwa niaba ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, Nawatakia Kumbukumbu Njema ya Miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika. Hongera Tanganyika, Hongera Tanzania! Amani na Maridhiano Daima.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Sheikh Dkt. Alhad Mussa Salum, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT-TAIFA), ametuma salamu na pongezi maridhawa kwa Watanzania wote katika mnasaba wa kuadhimisha siku muhimu ya Uhuru wa Tanganyika.

Ifuatayo ni nukuu ya Ujumbe wa Kiongozi huyo:

Kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu

Ndugu Watanzania wenzangu,
Leo tunakutana katika kumbukumbu adhimu na yenye uzito mkubwa katika historia ya Taifa letu - kumbukumbu ya Miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika, siku ambayo mnamo tarehe 9 Desemba 1961 wazalendo wetu waliliingiza taifa hili katika nuru ya uhuru kwa njia ya mazungumzo, busara na hekima, pasina kumwagika hata tone la damu.

Katika bara la Afrika ambapo mataifa mengi yalipitia mapambano makali ya kivitendo ili kufikia uhuru, Tanganyika iliweka historia ya kipekee kwa kusimama imara katika diplomasia, ustaarabu na utamaduni wa majadiliano. Hili lilitekelezwa kupitia uongozi mahiri wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na viongozi wengine wa TANU, waliolitanguliza taifa mbele ya maslahi binafsi.

Kwa hekima na msimamo thabiti, wakatangaza kwa dunia kwamba haki inaweza kupatikana pasina vita—na dunia ikashuhudia taifa jipya likizaliwa kwa amani.


Safari ya Uhuru: Msingi wa Taifa Imara

Kama Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, ninakumbusha kwamba misingi iliyowekwa na waasisi wa taifa hili ndiyo imeendelea kulifanya liwe kisiwa cha amani barani Afrika.

Siku hii inatukumbusha thamani ya:

1_Amani ambayo ndiyo nguzo kuu ya maendeleo yetu;

2_Mshikamano na undugu unaotuvusha changamoto nyingi kama taifa moja lisilo na mipasuko;

3_Heshima ya kitaifa na kimataifa tunayoendelea kupewa kutokana na msimamo wetu wa amani, maridhiano na utu.


Mienendo ya Maendeleo: Miaka 64 ya Safari

Tanganyika na baadaye Tanzania ya Muungano, imepitia hatua kubwa za maendeleo katika nyanja mbalimbali:

1_Elimu imepanuka kwa kasi, kutoka madarasa machache hadi mfumo mpana wa elimu kwa wote.

2_Afya imeimarika, huduma zimefika mbali vijijini.

3_Miundombinu imerekebisha sura ya taifa - barabara, reli, madaraja na teknolojia.

4_Diplomasia ya Tanzania imeendelea kuonyesha dira ya busara, amani, na uongozi barani Afrika.

5_Maendeleo ya kiuchumi na kijamii yanaendelea kupanda hatua kwa hatua.


Hakika safari ya Uhuru haikuishia mwaka 1961; ilianza miaka 64 iliyopita na inaendelea leo - tukiwa sisi ni wajumbe wa kuibeba mbele.

Jukumu la Kizazi Cha Leo: Kuilinda Amani Yetu

Katika dunia inayokumbwa na misukosuko ya kisiasa, vita, misimamo mikali na migogoro ya kijamii, Tanzania imesimama imara kama mfano wa kuigwa katika:

1_Mazungumzo na maridhiano,

2_Siasa zisizojenga chuki,

3_Uongozi wa kuvumiliana,

4_Utamaduni wa kuishi kama familia moja.

Nasisitiza kwa dhati kwamba kudumisha Amani ni wajibu wa kila raia, kiongozi, taasisi, na jumuiya zote za dini na kijamii. Bila Amani hakuna maendeleo, hakuna ustawi, na hakuna ustahimilivu wa taifa.


Kwa kuhitimisha

Kwa heshima kubwa, nawaalika Watanzania wenzangu kuendeleza dira ya taifa letu la Amani.

Tuendelee kuenzi urithi wa waasisi wetu, tuutunze uhuru wetu, na tuuendeleze kwa misingi ya maridhiano, maadili na uadilifu.

Tanganyika ilipata Uhuru kwa njia ya Amani; na sisi leo hii tunalo jukumu la kuuimarisha na kuurithisha kwa vizazi vijavyo.

Kwa niaba ya Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania,
Nawatakia Kumbukumbu Njema ya Miaka 64 ya Uhuru wa Tanganyika.

Hongera Tanganyika, Hongera Tanzania!

Amani na Maridhiano Daima.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha