Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Katika dakika za mwanzo za vita fupi lakini yenye uharibifu mkubwa, Israel ilivuka mstari mwekundu ambao kwa miongo kadhaa ilikuwa ikiuepuka: kuwaua waziwazi wanasayansi wakuu wa nyuklia wa Iran. Hatua hiyo ilitekelezwa kupitia mashambulizi yaliyoratibiwa kikamilifu ya kijeshi na kijasusi.
Uchunguzi wa pamoja wa gazeti la Washington Post na kipindi cha uchunguzi cha Frontline cha runinga ya Marekani (PBS) unaonyesha jinsi kampeni hiyo ilivyopangwa kwa umakini mkubwa, ilivyoongozwa kisiasa, na kutekelezwa kwa ukatili uliopimwa. Operesheni hiyo iliitwa kwa jina la siri “Narnia.”
Mnamo Juni mwaka uliopita, Israel ilianzisha kampeni pana ya kijeshi na kijasusi dhidi ya Iran, iliyojumuisha mashambulizi ya anga, oparesheni za ardhini za siri, na mauaji yaliyolengwa. Lengo lililotangazwa lilikuwa kuipooza programu ya nyuklia ya Iran.
Operesheni hii haikuwa sehemu ya pembeni ya shambulio kubwa la anga lililojulikana kama “Simba Anayechomoza”, lililofanyika tarehe 13 Juni kwa ushiriki wa zaidi ya ndege 200 za kivita za Israel dhidi ya Iran; bali, kwa mujibu wa Washington Post, ilikuwa kiini cha kimkakati na moyo wa mashambulizi hayo.
Israel ilitaja hatua hiyo kama shambulio la kujikinga dhidi ya kile ilichokiita tishio la uwepo wa programu ya nyuklia ya Iran, ikidai Tehran imeendeleza makombora ya masafa marefu yanayoweza kubeba vichwa vya nyuklia na kuilenga Israel ndani ya dakika chache. Iran, kwa upande wake, ilitaja mashambulizi hayo kuwa uchokozi hatari, uhalifu wa kivita, na tangazo la vita linalohitaji jibu kali.
Mkakati wa “kukata kichwa”
Ripoti ya Washington Post inaeleza kuwa huku dunia ikishuhudia nguzo za moshi zikifuka kutoka katika vituo vya urutubishaji wa urani vya Iran, vita nyingine ya kina na ya muda mrefu zaidi ilikuwa ikiendelea ndani ya majengo ya makazi ya Tehran.
Vita hiyo ilikuwa Operesheni Narnia—mpango uliopimwa kwa uangalifu na vyombo vya ujasusi vya Israel kwa ajili ya kuwaondoa wanasayansi mashuhuri wa nyuklia wa Iran, waliotazamwa na maafisa wa Israel na Marekani kuwa uti wa mgongo wa juhudi zozote za baadaye za Tehran kutengeneza bomu la nyuklia.
Operesheni hiyo ilianza alfajiri ya tarehe 23 Khordad 1404 (kalenda ya Iran), sambamba na mwanzo wa vita vya siku 12 kati ya Iran na Israel. Silaha za Israel zililenga majengo ya makazi mjini Tehran na kuwaua wanasayansi bingwa wa fizikia na uhandisi wa nyuklia wakiwa ndani ya nyumba zao.
Miongoni mwa mashahidi wa awali walikuwa Mohammad Mehdi Tehranchi, mwanafizikia wa nadharia na mtaalamu wa vilipuzi aliyekuwa chini ya vikwazo vya Marekani, na Fereydoun Abbasi, aliyekuwa rais wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran—ambaye hapo awali alinusurika jaribio la mauaji mwaka 2010. Israel baadaye ilitangaza kuwa katika siku ya kwanza na zilizofuata, wanasayansi 11 mashuhuri wa nyuklia waliuawa.
Mauaji haya yalikuwa sehemu ya kampeni pana ya “Simba Anayechomoza”, iliyolenga vituo vya nyuklia, miundombinu ya makombora, mifumo ya ulinzi wa anga, na makamanda wa kijeshi wa Iran.
Maafisa wa Israel na Marekani walisema lengo halikuwa tu kuharibu miundombinu, bali kurudisha nyuma programu ya nyuklia ya Iran kwa miaka kadhaa kwa kuangamiza kile Washington Post inakiita “mkusanyiko wa akili”—yaani kizazi cha wanasayansi wenye uwezo wa kugeuza urani iliyorutubishwa kuwa silaha ya nyuklia inayofanya kazi.
Uchunguzi unaonyesha kuwa Israel ilikuwa imejiandaa kwa muda mrefu kwa wakati huu. Vyombo vyake vya ujasusi vilikusanya kwa miongo kadhaa taarifa za kina kuhusu wanasayansi wa nyuklia wa Iran: kuanzia tafiti zao za kisayansi, ratiba za kila siku, makazi yao, hadi mitandao yao ya kijamii.
Kutoka kwenye orodha ya awali ya takribani wanasayansi 100, hatimaye karibu watu 12 walichaguliwa kama wasio na mbadala wa haraka.
Tofauti na mauaji ya awali yaliyotekelezwa kwa siri na kukanushwa rasmi, safari hii Israel ilikiri wazi uwajibikaji. Maafisa walitaja sababu kuwa ni kujiamini zaidi baada ya kudhoofisha mikono ya Iran—ikiwemo Hamas huko Gaza na Hizbullah nchini Lebanon—na pia kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad nchini Syria.
Vifo vya raia
Hata hivyo, operesheni hii ilisababisha vifo vingi vya raia. Washington Post kwa kushirikiana na tovuti ya uchunguzi ya Bellingcat zimethibitisha kuuawa kwa angalau raia 71 katika mashambulizi matano yanayohusiana na mauaji ya wanasayansi wa nyuklia.
Katika majengo ya makazi yanayojulikana kama “Makazi ya Maprofesa” mjini Tehran, raia 10 waliuawa, wakiwemo mtoto mchanga wa miezi miwili. Katika shambulizi jingine lililomlenga mwanasayansi Mohammad Reza Seddiqi Saber lakini likashindikana kutokana na kutokuwepo kwake, mwanawe wa miaka 17 aliuawa.
Maafisa wa Israel walidai walifanya kila wawezalo kupunguza madhara ya pembeni, lakini wakakiri hatari zinazotokana na kuwalenga watu katika maeneo ya makazi.
Iran iliituhumu Israel kwa kuwalenga raia kwa makusudi na kutangaza kuuawa kwa zaidi ya watu 1,000. Israel, kwa upande wake, ilisema mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yaliua Waisraeli 31 na kuharibu miundombinu ya kiraia.
Tathmini za kijasusi—kwa mujibu wa Washington Post—zinaonyesha kuwa hasara zilikuwa kubwa lakini hazikuamua matokeo ya mwisho. Maafisa wa Marekani, Israel na Shirika la Kimataifa la Nishati ya Atomiki (IAEA) wanakubaliana kuwa programu ya nyuklia ya Iran imerudishwa nyuma kwa miaka kadhaa, lakini haijaangamizwa.
Gazeti hilo linaongeza kuwa Iran bado inamiliki takribani pauni 900 za urani yenye urutubishaji wa asilimia 60, kiwango kinachokaribia matumizi ya kijeshi. Pia, baada ya vita, upatikanaji wa wakaguzi wa IAEA kwenye baadhi ya maeneo muhimu umepunguzwa.
Hadaa ya kidiplomasia
Sehemu inayofichua zaidi ya ripoti ni kiwango cha uratibu kati ya Benjamin Netanyahu, waziri mkuu wa Israel, na serikali ya Donald Trump.
Kwa mujibu wa Washington Post, vita hii ilitanguliwa na miezi ya ujanja wa kidiplomasia na hadaa. Netanyahu aliwasilisha kwa Trump hali nne za kushambulia Iran—kuanzia shambulio huru la Israel hadi oparesheni iliyoongozwa kikamilifu na Marekani.
Ingawa Trump alionekana kupendelea suluhu ya kidiplomasia, pande zote mbili ziliendelea kwa siri kupanga pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi, huku zikiigiza tofauti za kisiasa ili kuipotosha Tehran.
Ripoti pia inafichua kuwa mazungumzo ya nyuklia yaliyopangwa kufanyika tarehe 15 Juni yalikuwa njama ya kuilaza Iran.
Hata wakati mashambulizi yalipoanza, Marekani—kupitia wapatanishi wa Qatar—iliwasilisha pendekezo la mwisho lenye masharti magumu, ikiwemo kuondolewa kabisa kwa vikwazo kwa kubadilishana na kusambaratishwa kwa vituo vya urutubishaji na kusitishwa kwa uungaji mkono wa Iran kwa makundi ya silaha ya kikanda. Baada ya Iran kukataa, Marekani kwa idhini ya Trump iliingia moja kwa moja vitani na kupeleka ndege za kivita za B-2 Spirit kushambulia kituo cha chini ya ardhi cha Fordow.
Motisha ya kijiografia
Washington Post inaelezea msururu wa matukio ya kikanda kama “dhoruba kamili” iliyochochea Israel kushambulia Iran.
Kwanza, kuanguka kwa serikali ya Bashar al-Assad nchini Syria mwaka 2024, kulikata njia kuu ya ardhini ya Iran kuelekea washirika wake.
Pili, kudhoofika kwa Hizbullah nchini Lebanon na Hamas huko Gaza, jambo lililoiacha Iran bila vizuizi vyake vya jadi. Baada ya kuuawa shahidi Sayyid Hassan Nasrallah mwishoni mwa 2024 na kuharibiwa kwa mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ya S-300, majenerali wa Israel waliona fursa adimu ya kiutendaji.
Licha ya uharibifu mkubwa, mafanikio ya muda mrefu ya kampeni hii bado yana shaka. Taasisi ya Sayansi na Usalama wa Kimataifa mjini Washington imeelezea uharibifu wa vituo vya Natanz na Isfahan kuwa janga kubwa.
Mkurugenzi Mkuu wa IAEA, Rafael Grossi, alisema uwezo wa kimwili wa Iran wa kurutubisha urani umeharibiwa vibaya, lakini Tehran bado imeshikilia msimamo wake.
Kwa mujibu wa Washington Post, Ali Larijani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, amesema kuwa programu ya nyuklia ya Iran haiwezi kuangamizwa, kwa sababu maarifa hayawezi kuharibiwa kwa mabomu.
Wakati Iran ikiendelea kujenga upya na kupanua vituo vyake vya chini ya ardhi, uchunguzi huu unahitimisha kuwa mashambulizi ya Israel na Marekani huenda yamechelewesha malengo ya nyuklia ya Iran, lakini hayajatatua mzizi wa tatizo, na huenda hata yakalisukuma kurejea kwa nguvu zaidi na kwa siri zaidi siku zijazo.
Your Comment