Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), Ayatullah Reza Ramezani, amesema kuwa Imam Khomeini (r.a) aliifanya dini irejee kutoka pembezoni mwa maisha ya kijamii na kisiasa hadi kuwa kiini cha jamii na mfumo wa utawala, akibadilisha kabisa mtazamo wa dunia ya kisasa kuhusu nafasi ya dini.
Ayatullah Ramadhani aliyasema hayo katika hafla ya kusaini hati ya makubaliano ya ushirikiano kati ya Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) na Taasisi ya Kusimamia na Kuchapisha Kazi za Imam Khomeini (r.a), iliyofanyika Jumatatu, kwa kuhudhuriwa pia na Hujjatul-Islam wal-Muslimin Ali Kamsari, Mkuu wa taasisi hiyo.
Akielezea muktadha wa dunia ya kisasa, Ayatullah Ramadhani alisema kuwa jamii ya leo kwa muda mrefu imekuwa ikitawaliwa na fikra za kimaada na kiasili, hali iliyosababisha dini kupuuzwa si tu katika nchi za Magharibi bali pia katika baadhi ya nchi za Kiislamu.
Alifafanua kuwa kulikuwepo aina mbili za mitazamo hasi kuhusu dini:
Mtazamo wa kwanza ulikuwa wa kupinga dini kabisa, kama ilivyoshuhudiwa katika Umoja wa Kisovieti wa zamani, na mtazamo wa pili ulikuwa wa kisekula, ambao ulikubali dini lakini uliipunguza hadi masuala binafsi na ya kiibada pekee, bila kuipa nafasi katika jamii na utawala.
Imam Khomeini (r.a) na “Msimamo wa Tatu” wa Kihistoria
Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuwa katika mazingira hayo, wengi walidai kuwa mapinduzi ya kidini hayawezekani tena katika dunia ya kisasa. Hata hivyo, Imam Khomeini (r.a) alidhihirisha kivitendo “msimamo wa tatu”, akionyesha kuwa dini inaweza kuwa mhimili wa maisha binafsi, ya kijamii na hata ya kisiasa na kiutawala.
Aliongeza kuwa kwa mtazamo wa Imam Khomeini, dini si suala la mtu binafsi pekee bali ni mfumo kamili wa maisha, jambo linalodhihirika wazi katika maandiko ya Sahifa ya Imam, ambayo yanaweza kuchukuliwa kama katiba ya fikra hiyo.
Ujumla wa Haiba ya Imam Khomeini (r.a)
Ayatullah Ramezani alieleza kuwa Imam Khomeini (r.a) alikuwa na haiba ya kipekee iliyounganisha hekima, irfani (tasawwuf), fikra za kielimu, fiqhi na utawala. Alibainisha kuwa Imam hakuona fiqhi kama sheria za mtu binafsi pekee, bali aliichukulia kama falsafa ya vitendo ya utawala na ujenzi wa jamii.
Aidha, alitofautisha mtazamo wa Imam Khomeini na kauli maarufu ya Shahid Modarres aliyesema “dini ni siasa na siasa ni dini”, akisema Imam alienda mbali zaidi kwa kuunganisha sharia, tariqa, hakiqa na siasa katika mfumo mmoja usiotenganishika.
Kubatili Nadharia ya Kuto-wezekana kwa Utawala wa Kidini
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ahlul-Bayt (a.s) alisisitiza kuwa Imam Khomeini (r.a) alivunja kwa vitendo nadharia zilizodai kuwa utawala wa kidini hauwezekani katika zama za kisasa, na akathibitisha kuwa dini inaweza kuwa nguvu ya kujenga ustaarabu.
Aliongeza kuwa leo fikra za Imam Khomeini zinajadiliwa katika vyuo vikuu vikubwa duniani kama Sorbonne, Harvard, Cambridge na Oxford, huku wasomi wa Magharibi wakikiri kuwa mitazamo ya Madhehebu ya Ahlul-Bayt (a.s) ina uwezo wa kujibu maswali ya msingi ya mwanadamu wa leo.
Umuhimu wa Kuutambulisha Ulimwenguni Ufikra wa Imam
Ayatullah Ramadhani alisisitiza umuhimu wa kuitambulisha dunia Imam Khomeini kwa sura yake kamili, si kama kiongozi wa kisiasa pekee bali pia kama mfasiri wa Tauhidi, mtetezi wa haki za kijamii na mwanairfani mkubwa.
Alibainisha kuwa kwa masikitiko, katika sehemu nyingi za dunia Imam anatambulika kisiasa tu, ilhali vipengele vyake vya kiroho na kimaarifa havijatambuliwa ipasavyo. Alitoa mfano wa uzoefu wake katika vyuo vikuu vya Ufaransa, ambako kujadili irfani ya Imam kuliwafanya wasikilizaji wagundue sura mpya kabisa ya Imam Khomeini.
Maudhui ya Makubaliano ya Ushirikiano
Mwisho, Ayatullah Ramadhani alieleza kuwa makubaliano hayo yanahusisha:
1_Tafsiri na uchapishaji wa kazi za pamoja
2_Uzalishaji wa maudhui ya kielimu na vyombo vya habari
3_Programu za kielimu, makongamano na mijadala ya kitaaluma
4_Uundaji wa majukwaa ya mawasiliano na wasomi wa kimataifa.
Akihitimisha, alieleza matumaini kuwa makubaliano hayo yatakuwa kielelezo cha ushirikiano wenye mafanikio katika kueneza fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na Maktaba ya Ahlul-Bayt (a.s) duniani.
Your Comment