4 Oktoba 2012 - 09:42

Uturuki inalitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuichukulia hatua serikali ya Syria baada ya majeshi yake kuishambulia kwa makombora na kuua raia wake watano mjini Akcakala siku ya Jumatano.

Hatua hiyo ilisababisha Uturuki kulipiza kisasi kwa kurusha makombora yake  nchini Syria na kusababisha mauaji ya wanajeshi wa serikali kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Syria.

Uhusiano kati ya mataifa hayo mawili ulianza kutetereka mwezi Juni baada ya Syria kudungua ndege ya kijeshi ya Uturuki na kusababisha vifo ya marubani wake.

Uturuki imeendelea kuituhumu Syria kwa kutoheshimu sheria za kimataifa kwa kuingia katika mipaka yake na kusababisha mashambulizi jambo ambalo Uturuki inasema haitavumilia tena.

Bunge nchini Uturuki linakutana siku ya Alhamisi kujadili  hatua zaidi  dhidi ya serikali ya Damascus ambayo tayari imeonesha kusikitishwa kwake na mauaji ya raia wa Uturuki.

Uongozi wa majeshi ya kimataifa NATO, yameshtumu hatua hiyo ya Syria na kuongeza kuwa itaendelea kusimama na serikali ya Uturuki.

Wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanakutana Alhamisi kujadiliana hatua hiyo ya Syria na kushtumu kitendo hicho cha kuishambulia Uturuki.

Serikali ya Uturuki imeendelea kusisitiza kuwa rais Bashar Al Assad ni sharti aondoke mamlakani msimamo ambao serikali ya Damascus imesema Uturuki inaunga mkono magaidi nchini mwake.