20 Desemba 2014 - 09:35
Rais wa Kenya apitisha sheria kali dhidi ya ugaidi

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria mswada wenye utata wenye lengo la kupambana na ugaidi na kusababisha wabunge kutupiana ngumi bungeni na kuzusha madai kuwa unakiuka misingi ya uhuru

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametia saini kuwa sheria mswada wenye utata wenye lengo la kupambana na ugaidi na kusababisha wabunge kutupiana ngumi bungeni na kuzusha madai kuwa unakiuka misingi ya uhuru

Kenyatta amesema ameridhishwa kwamba mswada huo umepitishwa na bunge la taifa siku ya Alhamis na haukiuki katiba ya nchi hiyo. "Wasi wasi wote uliooneshwa na wadau tofauti umeshughulikiwa na kamati zinazohusika za bunge," amewaambia waandishi habari, na kuwataka Wakenya wote kusoma sheria hiyo mpya na kuamua wao binafsi.

"Lengo lake ni moja - moja tu- kulinda maisha na mali za raia wote wa jamhuri ya Kenya," amesema rais Kenyatta.

Sheria hiyo mpya inatoa kwa maafisa wa madaraka makubwa kuwasaka watuhumiwa wa ugaidi na kuweka mipaka kwa uhuru wa vyombo vya habari katika nchi ambayo tayari imeathirika na wimbi la mashambulio yanayofanywa na kundi la al-Shabaab kutoka nchi Somalia lenye mafungamano na kundi la kigaidi la al-Qaeda.

Hatua hizo zenye utata zinaongeza muda wa polisi kuwashikilia watuhumiwa wa ugaidi kutoka siku 90 za sasa hadi karibu mwaka mmoja na kuongeza hukumu inayowakabili.

Wakati huo huo, waandishi habari wanaweza kukabiliwa na hukumu ya hadi kifungo cha miaka mitatu iwapo ripoti zao zitaingilia uchunguzi ama operesheni za usalama zinazohusika na ugaidi", ama iwapo watachapisha picha za wahanga wa ugaidi bila ya ruhusa ya polisi.

Serikali inadai kuwa hatua hizo ni muhimu kuweza kupambana na wanamgambo na inasema mabadiliko ya katiba ya msingi, na kutoa kwa mahakama nafasi kubwa zaidi kwa polisi na idara za usalama, ni sahihi kikatiba.

Upinzani na makundi ya haki za binadamu , hata hivyo, wanakataa mabadiliko hayo na kusema ni kisingizio na wanadai sheria hiyo inahatarisha kuigeuza Kenya kuwa taifa la kipolisi.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Marekani Jen Psaki amesema Marekani "inaiunga mkono kwa dhati Kenya katika juhudi zake za kulishinda kundi la al-Shabaab na kuhakikisha usalama wa raia zake.

Hata hivyo, licha ya kuwa sheria hizo "zimelenga kuongeza uwezo wa Kenya kuzuwia na kuwashinda magaidi," Psaki amesema, "tunakatishwa tamaa kwamba sheria hiyo muhimu haikupewa muda wa kutosha kwa ajili ya kuijadili kwa kina."

"Tunaitaka serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba juhudi zake za kupambana na ugaidi zinaheshimu haki za Wakenya wote na kuheshimu katiba na utawala wa sheria," Psaki amesema.

Mgawanyiko kuhusu sheria hizo umezusha vurugu bungeni siku ya Alhamis. Wabunge wa upinzani walichana nakala za mswada huo na kurushiana makonde na wale wanaounga mkono mswada huo, na kulazimisha kura hiyo kucheleweshwa kwa kipindi cha muda flani.

Kenyatta ameshutumu hali hiyo na kusema, ni ya "kusikitisha" na kuwashutumu wapinzani kwa kutotambua kitisho kinachoikabili nchi hiyo kwa wakati huu.

Tags