Maafisa wa Afghanistan wamesema wanajeshi wanne wameuawa katika mapigano ya kuzuia shambulizi la Wataliban kwenye kituo cha jeshi cha ukaguzi wa barabarani katika mkoa wa Helmand wenye visa vingi vya vurugu.
Msemaji wa gavana wa jimbo hilo Omar Zwak amesema wanajeshi wengine watatu walijeruhiwa katika makabiliano hayo yaliyotokea jana jioni katika wilaya ya Sangin. Msemaji huyo amesema kuwa wapiganaji wanane wa Taliban pia waliuawa. Kundi la Taliban limetangaza kuhusika na mashambulizi hayo.
Wilaya ya Sangin imeshuhudia mapigano makali kati ya wanajeshi wa serikali na wataliban mnamo miezi sita iliyofuatia kuondoka kwa wanajeshi wa Umoja wa Kujihami, NATO. Kuwepo kwa wanajeshi wa Marekani na wenzao kutoka nchi nyingine wanachama wa NATO kunamalizika rasmi wiki hii baada ya kuwepo nchini Afghanistan kwa muda wa miaka 13.
Weledi wa mambo wanasema kuwa majeshi ya Marekani na NATO yameshindwa kupambana na kikundi cha kigaidi cha Taleban pamoja na kuwepo majeshi ya nchi hizo katika ardhi ya Afghanistan kwa muda wa miaka kumi na tatu.