Polisi ya Ufaransa Jumamosi ya leo iko kwenye msako mkali wa mjane wa mmojawapo wa watuhumiwa waliouwawa waliohusika na wimbi la mashambulizi mjini Paris ambaye binafsi anahesabiwa kuwa ni mtu wa hatari sana.
Akiwa na silaha ya upinde mikononi mwake na akiwa amevalia bui bui lililomfunika gubi gubi na kuwacha wazi sehemu ya macho tu hii ndio ilikuwa taswira ambayo hivi sasa imesambazwa ya mwanamke anayesakwa kwa udi na uvumba nchini Ufaransa anayeitwa Hayat Boumeddiene.
Mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 26 ni mke wa Amedy Coulibaly mmojawapo wa watu watatu waliokuwa na silaha ambao wameuwawa kwa kupigwa risasi na polisi baada ya siku tatu za purukushani nchini Ufaransa.
Picha hiyo ambayo mara ya kwanza ilichapishwa na gazeti la Le Monde tafauti na ile ambayo polisi ya Ufaransa iliitowa katika wito wake wa kwanza wa kumtafuta alipo kufuatia kisa cha umwagaji damu hapo Ijumaa ambapo Colibaly aliuwawa na makamandoo wa polisi baada ya kuwashikilia watu mateka katika duka moja Kiyahudi mjini Paris.
Picha hiyo iliyotolewa na polisi inamuonyesha kijana wa kike mwenye macho ya kusinzia uso wake na nywele zake za kahawia zikiwa wazi wakati walipomhoji hapo mwaka 2010 kuhusu Coulibaly.
Hata hivyo ilani hiyo ya polisi ilionya kwamba mwanamke huyo anahesabiwa kuwa ni hatari na kwamba alikuwa na silaha.
Anatuhumiwa kuwa alikuwa pamoja na Coulibaly katika mauaji ya polisi wa kike kusini mwa Paris hapo Alhamisi wakati wa msako mkubwa wa ndugu wawili ambao siku moja kabla walifanya mauaji makubwa ya watu kumi na mbili katika ofisi ya gazeti la vichekesho litolewalo kila wiki la Charlie Hebdo.
Polisi inashuku kwamba yumkini akawa na mkono wake katika tukio la kushikilia watu mateka katika duka lililofanywa na Coulibaly juu ya kwamba alikuwa hakuweza kutambulikana miongoni mwa watu waliokufa au majeruhi.
Coulibaly mwenye umri wa miaka 32 alikuwa ni mhalifu wa muda mrefu ambaye inaonekana kuwa aligeuka kuwa Muislamu wa itikadi kali wakati akiwa akitumikia vifungo gerezani.
Alidai katika simu aliyopiga kwa muda mfupi kwa kituo cha televisheni cha Ufaransa BFMTV wakati akiwa kwenye sakata hilo la kuzingirwa kwa duka alikokuwa akiwashikilia watu mateka kwamba alikuwemo katika kundi la wapiganaji wa jihadi la Daesh.
Coulibaly pia amesema kwamba alikuwa ameratibu hatua yake hiyo ya kuwashikilia watu mateka na wale wanaume wengine wawili wenye silaha ambao ni ndugu Cherif na Said Kouachi ambao nao walidai kwa nyakati tafauti kwa kituo cha BMFTV kwamba wamo kwenye kundi jengine la itikadi kali la Al Qaeda nchini Yemen.
Cherif Kouachi raia wa Ufaransa mwenye asili ya Algeria na mwenye umri wa miaka 32 inasemekana alimshinikiza Colibaly ambaye pia ni raia wa Ufaransa kuingia kwenye msimamo mkali wa dini ya Kiislamu wakati walipokuwa gerezani pamoja.
Kwa mujibu wa mwendesha mashtaka wa mji wa Paris Francois Molins uhusiano kati ya Coulibaly na akina Kouachi ulikuja kubainika kwa serikali baada ya kugunduwa kwamba Boumeddiene na mwanamke wa mmojawapo wa ndugu akina Kouachi waliwasiliana kwa simu zaidi ya mara 500 hapo mwaka 2014.
Wapelelezi hivi sasa wanazipekuwa rekodi za simu na na vitu vyengine vilivyokamatwa wakati wa kusachi kuyakinisha kiwango cha ushirikiano wao na mtu mwengine yoyote yule ambaye yumkini akawa ana husika na watu hao.
Lakini kwa sasa nadhari iko kwa Bomeddiene.
Colibaly aliishi pamoja na mwanamke huyo hapo mwezi wa Mei mwaka jana wakati alipoachiliwa kutoka katika kifungo chake cha mwisho gerezani.
Boumeddine ambaye ni miongoni mwa watoto saba ambaye mama yake alifariki akiwa na umri na miaka sita alikuwa akilelewa katika nyumba za kutunza watoto pamoja na ndugu zake wadogo kwa sababu baba yake aliyekuwa akifaya kazi ya kuwasilisha vifurushi hakumudu kuwatunza.
Alifunga ndoa ya kidini na Coulibaly hapo mwaka 2009 juu ya kwamba ndoa za aina hiyo huwa hazitambuliwi nchini Ufaransa venginevyo zinatanguliwa na ndoa za kiraia zinazosimamiwa na maafisa wa serikali na wanandoa hao walikuwa wakiishi katika nyumba ya wastani katika kitongoji cha kimaskini kusini mwa Ufaransa.
Gazeti la Le Parisian limesema alipoteza kazi yake akiwa kama mpokea malipo kwa sababu alikuwa akisisitiza kuvaa bui bui lake linalomfunika gubi gubi vazi la Kiislamu linalojulikana kwa jina la niqab.
Boumeddiene amekuwa akiandamana na Coulibaly mara kwa mara kwenda msituni eneo la kati kusini Ufaransa kutunga shabaha ya upinde.Le Monde limechapisha picha kadhaa za wanandoa hao wakishikilia silaha hiyo ya upinde huku Boumeddiene akiwa amevalia bui bui lake hilo.
Mahala aliko hakujulikani lakini maelfu ya polisi wamemwagwa kumsaka.