10 Januari 2015 - 19:26
Hofu ya mashambulizi mengine ya kigaidi yatanda Ufaransa

Ufaransa imeelezea hofu juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi mengine ya kigaidi nchini humo, baada ya yale yaliyotokea wiki hii mjini Paris

Ufaransa imeelezea hofu juu ya uwezekano wa kutokea mashambulizi mengine ya kigaidi nchini humo, baada ya yale yaliyotokea wiki hii mjini Paris. Makundi mawili ya kigaidi; al-Qaida na Daesh, yametishia kufanya mashambulizi dhidi ya Ufaransa na nchi nyingine za Ulaya.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ametoa tahadhari kwamba bado nchi yake inakabiliwa na kitisho, na Marekani imewataka raia wake wanaotembelea nchi za nje kuchukua hatua muafaka kuhakikisha usalama wao. Ufaransa imetangaza hali ya tahadhari kubwa mjini Paris, ambako kesho yatafanyika maandamano na mazishi ya wahanga wa mashambulizi ya kigaidi ya wiki hii.

Viongozi wengi wa Ulaya akiwemo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel watashiriki katika maandamano hayo. Jana jioni kikosi maalumu cha polisi ya Ufaransa kiliwauwa ndugu wawili walioishambulia ofisi ya jarida la Vibonzo la Charlie Hebdo na kuuwa watu 12. Pia kilimuuwa mtekaji nyara mwingine katika duka la vyakula la kiyahudi, ambaye siku iliyotangulia alikuwa amemuuwa afisa wa polisi. Mke wake bado anatafutwa na polisi.

Ufaransa ni moja kati ya nchi ambazp hapo awali zilikuwa zikiyaunga mkono makundi ya kigaidi yanayopambana dhidi ya serikali ya Syria kwa malengo ya kuiangusha serikali ya Bashar asad na inahesabika kuwa ni nchi yenye raia wengi zaidi waliojiunga katika kundi la kigaidi la Daesh linalofanya jinai zake Syria na Iraq.

 

Tags