Viongozi wa dunia wameshikana mikono kuwaongoza mamia ya wananchi wa Ufaransa katika maandamano yaliokuwa chini ya ulinzi mkali kutowa heshima zao kwa wahanga wa mashambulizi ya wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali ambao walishambulia ofisi ya gazeti iliyo mdhalilisha mtume Muhammad s.a.w.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa aliandamana bega kwa bega na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ambao walikuwa mstari wa mbele pamoja na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas.
"Paris leo ni mji mkuu wa dunia" amesema hayo Rais Hollande kabla ya kuanza safari ya maandamano yaliohudhuriwa na watu milioni moja na nusu mjini Paris.Maandamano kama hayo ya kulaani ugaidi yamefanyika katika miji mengine nchini kote Ufaransa na Ulaya.
Polisi na wanajeshi wanaofikia 2,200 walikuwa katika doria kwenye mitaa ya Paris kuwalinda waandamanaji dhidi ya uwezekano wa kushambuliwa huku polisi wa kulenga shabaha wakiwa wamemwagwa kwenye mapaa ya nyumba na askari kanzu wakichanganyika na umati wa watu.
Maandamano hayo ambayo yamkini yakawa ndio maandamano makubwa kabisa katika historia ya kisiasa kufanyika Paris yanaonyesha fadhaa iliyotokana na shambulio baya kabisa la wanamgambo wa Kiislamu wa itikadi kali kuwahi kushuhudiwa katika mji mkuu wa Ulaya katika kipindi cha miaka tisa.
Kwa Ufaransa yamezusha masuala ya uhuru wa kujieleza,dini na usalama na kutoka nje ya mipaka ya Ufaransa mashambulizi hayo ya kigaidi yameonyesha urahisi wa kufanyika kwa mashambulizi hayo mijini.
Watu wawili waliohusika na mashambulizi hayo wametangaza utiifu wao kwa kundi la Al Qaeda lilioko Yemen na mshambuliaji wa tatu ametangaza utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh ambalo linafanya jinai zake huko Iraq na Syria.
Watu 17 wakiwemo waandishi na polisi wameuwawa katika siku tatu za matumizi ya nguvu ambayo yalianzia na shambulio la mauaji dhidi ya ofisi ya gazeti la kila wiki la Charlie Hebdo linalojulikana kwa tashtiti zake kwa Uislamu na dini nyengine pamoja na wanasiasa, waandishi wa gazeti hili ndio sababu kuu ya kutokea shambulio hilo na kusababisha watu wasio na hatia kuuawa, kwani walichora makatuni na kuyanasibisha na mtume Muhammad s.a.w jambo ambalo liliwaudhi viongozi wa makundi ya kigaidi na kufanya mauaji hayo, ambayo wamesema kuwa iwe ni somo kwa wengine wenye fikra mbovu za kumdhalilisha mtume wao.
Taharuki hiyo ilimalizika Ijumaa kwa ushikiliaji wa mateka katika duka moja la Kiyahudi ambapo mateka wanne waliuwawa pamoja na mhusika wa kisa hicho ambaye aliuliwa na polisi.
Muda mfupi kabla ya kuanza kwa maandamano kumeibuka mkanda wa video wenye kumuonyesha mwanaume anayefanana na yule aliyehusika na kisa cha kuwashikilia watu mateka katika duka la Kiyahudi akiahidi utiifu wake kwa kundi la kigaidi la Daesh na kuwataka Waislamu wa Ufaransa kufuata mfano wake.
"Hatutokubali kuliachia genge la wahuni kuyaendesha maisha yetu" hayo yametamkwa na Fanny Applebaum mwenye umri wa miaka 75 ambaye amesema alipoteza dada zake wawili na kaka mmoja katika kambi ya mateso ya Manazi huko Auschwitz.Amesema "Leo sote ni kitu kimoja".
Zakaria Moumni raia wa Ufaransa mwenye asili ya Moroco ambaye ana umri wa miaka 34 aliyejifunika kwa bendera ya Ufaransa amekubaliana na kauli hiyo kwa kusema kwamba “Niko hapa kuwaonyesha magaidi hawakushinda....ni kuwajumuisha pamoja watu wa dini zote."
Miongoni mwa watoto wengi waliopelekwa kwenye maandamano hayo ni Loris Peres mwenye umri wa miaka 12 aliyesema "Kwangu mimi huku ni kutowa heshima kwa watu unaowapenda ni kama familia ......tuliwahi kuwa na somo kama hilo shuleni."
Wakati kukukiwa na mshikamano mkubwa na wahanga pia kumekuwepo na sauti za upinzani.Mitandao ya kijamii nchini Ufaransa imekuwa na matamshi kutoka kwa wale ambao wana mashaka na kauli mbiu ya "Je suits Charlie" ikitafsiriwa kama ni uhuru wa kujieleza kwa gharama zozote zile. Wengine wanashuku kwamba kuna unafiki kwa viongozi wa dunia wanaohudhuria maandamano hayo ambao nchi zao zina sheria za kukandamiza vyomvbo vya habari.
Watu 12 waliuwawa katika shambulio la kwanza Jumatano dhidi ya ofisi ya gazeti la Charlie Hebdo kijarida kinachojulikana kwa kudhalilisha dini, viongozi wa dini, mitume na wanasiasa.Washambuliaji ndugu wawili wazawa wa Ufaransa wenye asili ya Algeria wameshambulia ofisi ya jarida hilo kwa kuchapisha katuni zenye kumfananiza na kumdhihaki Mtume Muhammad s.a.w.
Pamoja na kutokea maandamano kadha wa kadha ya wafuasi wa dini ya kiislamu wakipinga kuwa hawaruhusu mtu yeyote kuchezea matukufu ya dini yao, bado tunaendelea kushuhudia matukio ya kushangaza ambapo wengine wamechoma moto Qur an na wengine wanachora vibonzo na vikatuni kumdhalilisha mtume wa uislamu Muhammad s.a.w.
Weledi wa mambo wanazishauri nchi za Ulaya na nchi nyingine kote duniani ziheshimu matukufu ya dini nyingine hasa dini ya kiislamu ambayo haitaki dhihaka tofauti na dini nyingine, ili kuepukana na mashambulizi yanayoleta madhara kwa wengi ambayo hayana msingi wa kiakili.
Ufaransa ni moja kati ya nchi ambazo zilikuwa zikiwaunga mkono magaidi wa Daesh ili kuiangusha serikali ya Syria na imetuma wapiganaji wengi katika nchi hiyo ambao wanapambana chini ya kikundi cha kigaidi cha Daesh.