Katika maelezo yaliyojaa mazingatio, khatibu alibainisha kuwa Moto wa Jahannamu una mawe yanayochoma hadi kufikia ubongo wa waliomo ndani yake, na kwamba kila aina ya moto ni adhabu maalumu kwa aina fulani ya dhambi, kama zilivyobainishwa katika Hadithi za Mtume.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Waumini wa Kiislamu wakiwemo wanafunzi wa elimu ya dini, walimu waheshimiwa pamoja na waumini wa eneo hilo, walishiriki Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msala wa Shule ya Imam Al-Hadi (as) ambapo Sheikh Abdulrahman Kachera alikuwa Khatibu na Imam wa Sala ya Ijumaa.
Katika khutba yake yenye mawaidha mazito, Sheikh Kachera alizungumzia kwa kina Mada ya Jahannamu (Moto wa Akhera) na Baadhi ya Sifa Zake, akisisitiza umuhimu wa kumuogopa Mwenyezi Mungu na kujiepusha na dhambi.
Sheikh alieleza kuwa ukafiri ni miongoni mwa sababu kuu zitakazowapeleka watu Jahannamu, kwa mujibu wa Aya mbalimbali za Qur’ani Tukufu. Aidha, alifafanua kuwa Jahannamu lina majina mengi tofauti, jambo linaloonesha uzito na ukubwa wa adhabu yake.
Katika ufafanuzi wake, alieleza pia kuwa moto wa Jahannamu una nguvu mara 70 zaidi ya moto wa duniani, kama zilivyopokelewa katika Hadithi za Mtume Muhammad (s.a.w.w). Aliongeza kuwa Jahannamu lina milango saba ya kuingilia, nayo pia imegawanyika kwa makundi ya watu kulingana na aina za dhambi zao.

Sheikh Kachera alisisitiza kuwa Jahannamu lina tabaka saba, ambapo kila tabaka limeandaliwa kwa adhabu ya aina maalumu ya dhambi. Alifafanua kuwa Sa‘ir ni tabaka la sita, huku Jahannamu ikiwa tabaka la mwisho na lenye adhabu kali zaidi.
Katika maelezo yaliyojaa mazingatio, khatibu huyo alibainisha kuwa Moto wa Jahannamu una mawe yanayochoma hadi kufikia ubongo wa waliomo ndani yake, na kwamba kila aina ya moto ni adhabu maalumu kwa aina fulani ya dhambi, kama zilivyobainishwa katika Hadithi za Mtume(s.a.w.w).

Aidha, alieleza kuwa wakazi wa Jahannamu watakuwa na mavazi yaliyoshonwa kwa moto, na watapewa chakula na vinywaji vilivyotengenezwa kwa moto, ambavyo ni vya mateso makali, kama Qur’ani Tukufu inavyobainisha.
Sheikh Kachera alihitimisha khutba yake kwa kuwataka waumini kurejea kwa Mwenyezi Mungu, kuimarisha ibada, kutekeleza mema na kujiepusha na maasi, ili kuepuka adhabu hiyo kali ya Akhera.
Sala hiyo ya Ijumaa ilimalizika kwa dua maalum ya kuwaombea Waislamu wote wa dunia, hususan wale wanaokabiliwa na misukosuko na dhulma katika maeneo mbalimbali.


Your Comment