Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Wamarekani waliokuwa na hasira waliendelea kuonyesha hasira na upinzani wao dhidi ya mauaji yaliyofanywa na polisi mzungu dhidi ya raia mwenye asili ya Afrika, George Floyd, huko katika mji wa Minneapolis kwa kuvunja sanamu la rais wa kwanza wa Marekani, George Washington katika mji wa Portland jimbo la Oregon na kisha wakachoma moto kichwa chake.
George Washington anatambuliwa kuwa mwasisi wa Marekani na rais wa kwanza wa nchi hiyo.
Siku chache zilizopita pia waandamanaji waliokuwa na hasira walivunja sanamu jingine la George Washington lililokuwa karibu na ikulu ya rais wa Marekani, White House na katika mji uliopewa jina lake wa Washington DC.
Hadi sasa makumi ya masanamu ambayo yalikuwa nembo za kipindi au vinara wa biashara ya utumwa wa Marekani yamebomolewa katika maandamano yanayoendelea nchini humo kupinga ubaguzi wa rangi unaofanyika kwa mpangilio maalumu.
Miongoni mwa masanamu yaliyovunjwa ni lile la Christopher Columbus, mzungu kutoka Ulaya aliyedai kuvumbua bara Amerika na sanamu la Edward Colston aliyekuwa mfanyabiashara wa watumwa katika karne ya 17.
Waandamanaji wanaopinga ubaguzi wa rangi nchini Marekani wamebomoa, kuharibu na kuvunja vichwa vya sanamu la Christopher Columbus kuanzia miji ya Boston upande wa kaskazini hadi Miami huko kusini.
Wanasiasa wengi nchini Marekani wametoa wito wa kuondolewa alama zote zinazowakilisha wakoloni na wamiliki watumwa baada ya maandamano yaliyochochewa na mauaji ya George Floyd wiki kadhaa zilizopita.
Spika wa Baraza la Wawakilishi Nancy Pelosi ametaka kuondolewa kwa masanamu makubwa 11 ya wanajeshi na maafisa wa enzi za vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Marekani mwaka 1861 hadi 1865.
Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump amekaidi pendekezo hilo na kusisitiza kwamba, hatafikiria kubadilisha majina ya kambi za kijeshi ambazo zimepewa majina ya majenerali wabaguzi wa rangi na ambao waliunga mkono utumwa.
342/