Shirika la habari la Ahlubayt (as)ABNA: Mauaji ya Kfar Qasim ni miongoni mwa jinai za kutisha ambazo kamwe hazitasahauliwa na watu wa Palestina na ulimwengu kwa ujumla. Mauaji hayo yalifanyika tarehe 29 Oktoba mwaka 1956. Siku hiyo polisi na askari wa Israel waliwashambulia wakazi wa kijiji cha Kfar Qasim kilichoko kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu na kuwaua shahidi Wapalestina 49 wakiwemo wanawake 6 na watoto 23.
Kuhusu jinai hiyo ya Wazayuni tunapaswa kuashiria nukta muhimu kadhaa:
Kwanza ni kuwa, jinai hiyo ilifanyika katika siku ya kwanza ya vita vya Waarabu na Israel mwaka 1956. Mauaji hayo yalifanywa tarehe 29 Oktoba 1956 masaa kadhaa kabla ya mashambulizi yya pande tatu ya Israel, Ufaransa na Uingereza dhidi ya Misri ili kujibu hatua ya Cairo ya kutaifisha Mfereji wa Suez. Jinai hiyo ilifanyika wakati wakazi wa Kfar Qasim hawakuwa na habari kwamba utawala huo haramu umetangaza serikali ya kijeshi katika eneo hilo. Wakati wanawake na watoto walipokuwa wakirejea majumbani mwao jioni ya tarehe 29 Oktoba 1956, polisi na askari wa Israel waliwamiminia risasi bila ya kujali vilio na sauti za watoto hao waliokuwa wakiomba msaada.
Pili ni kwamba, serikali ya Israel ilifanya jitihada kubwa za kuficha jinai na ukatili huo ambao ulikuja kufichuliwa baadaye na wanachama wawili wa Knisset. Tawfiq Touba na Meir Flanner walifanikiwa kukusanya ushahidi na matamshi ya manusura wa mauaji hayo na kuyavujisha katika vyombo vya habari vya kimataifa.
Tatu ni kwamba, baada ya kuzidi mashinikizo ya kimataifa, serikali ya utawala dhalimu wa Israel ilifanya jitihada za kupunguza mashinikio hayo na kujitoa kimasomaso kwa kuwahukumu kimaonyeho tu baadhi ya askari walioshiriki katika ukatili na mauaji hayo. Mahakama ya Israel iliwahukumu viongozi walioamuru mauaji hayo kutoa fidia ndogo ya pesa. Baadaye mahakama hiyo hiyo iliwasamehe makatili wa mauaji hayo na hatimaye faili hilo likafungwa.
Nne ni kwamba, lengo la mauaji hayo lilikuwa kutekeleza mauji ya kimbari na kufuta kabisa uwepo wa Wapalestina katika kijiji cha Kfar Qasim. Kwa hakika utawala huo ulikusudia kuwafukuza kabisa wakati wa Kipalestina wa kijiji hicho, suala ambalo linapingana na sheria za kimataifa.
Tano ni kuwa, miaka 65 sasa baada ya mauaji ya kutisha ya Kfar Qasim rais wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Isaac Herzog amejitokeza hadharani na kuziomba radhi familia za wahanga wa ukatili huo. Herzog amesema: "Ninainamisha kichwa changu mbele ya kumbukumbu ya wahanga 49. Ninainamisha kichwa changu mbele yenu, familia zao, na mbele ya wakazi wa Kfar Qasim na kwa niaba yangu na Taifa la Israeli, ninaomba msamaha."
Matamshi haya ya Isaac Herzog ni kukiri kwa kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Israel kwamba utawala huo ulifanya jinai na mauaji ya kimbari, suala ambalo utawala huo haukuwa tayari kulifanya hadi hiyo jana. Sasa serikali ya Palestina inaweza kuwasilisha mashtaka katika mahakama za kimataifa na kwa uchache kutaka fidia ya ukati na mauaji hayo ya kinyama kwa ajili ya wakazi wa kijiji cha Kfar Qasim.
Nukta ya mwisho ni kuwa, katika maandamano yao ya jana huko Kfar Qasim wananchi wa Palestina walibeba bendera za rangi nyeusi na bendera za Palestina wakikumbuka tukio hilo la kusikitisha. Hii ni ishara kwamba, raia hao bado hawajasahau ukatili huo licha ya kupita miaka 65 baada ya jinai hiyo.
342/