Main Title

source : Parstoday
Jumamosi

24 Septemba 2022

15:37:45
1307807

Rais Mohamud: Somalia imejitolea vilivyo kukabiliana na njaa na ugaidi

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia ametoa mwito kwa washirika wa kimataifa kulisaidia taifa hilo la Pembe ya Afrika kupambana na baa la njaa na kuushinda ugaidi akisema kuwa serikali yake imedhamiria kikwelikweli kupambana na mambo hayo.

Katika sehemu moja ya hotuba yake mbele ya kikao cha 77 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Rais Mohamud amesema: Nchini Somalia, tunafanya kazi kwa bidii ili kuvuka kigingi cha zaidi ya miongo miwili ya mizozo mibaya, ukame, njaa na kudorora maendeleo.

Tuna matumaini juhudi zetu zitatupeleka hadi kwenye enzi mpya ya utulivu, maendeleo na ustawi. Lakini amesema, licha ya juhudi zetu zinazoendelea, Somalia na watu wake walio imara wanakabiliwa na migogoro tata zaidi iliyowahi kushuhudiwa duniani. Ameitaja migogoro hiyo kuwa ni pamoja na ukame unaoendelea wa kikanda, ambao unatishia moja kwa moja maisha ya jamii zilizoko hatarini zaidi za Somalia.

Katika ripoti mpya iliyotolewa Jumatano, Umoja wa Mataifa ulionya kuwa mamia kwa maelfu ya watu nchini Somalia tayari wanakabiliwa na njaa huku viwango vya juu vya utapiamlo miongoni mwa watoto walio chini ya miaka mitano vikitarajiwa kuongezeka.

Hii ni mara ya tatu katika kipindi cha miaka 10 ambapo Somalia imekumbwa na hatari ya kutumbukia kwenye baa la njaa.

Rais Mohamud alitoa wito kwa washirika wa Somalia kufanya kila linalowezekana kuisaidia nchi hiyo kuepusha janga hilo njaa ambalo pia linatishia eneo kubwa la Pembe ya Afrika. Somalia kwa mara ya kwanza imeanzisha wizara mpya ya mazingira na mabadiliko ya hali ya hewa ili kusimamia haraka mchakato wa kukabiliana na athari mbaya ya uharibifu wa mazingira. 

Wakati huo huo, Somalia inakabiliana na "changamoto inayoendelea na ngumu" ya ugaidi, ambayo Rais Mohamud amesema, changamoto hiyo inachangia na kuzidisha machafuko mengine yote, ikiwa ni pamoja na uhaba wa chakula na wimbi la wakimbizi kutokana na watu kulazimika kukimbia makazi yao na uharibifu wa mazingira.

342/