Main Title

source : Parstoday
Jumatano

5 Oktoba 2022

15:41:47
1310804

UN: Kuna ubaguzi wa rangi wa kimfumo dhidi ya watu weusi nchini Uswisi

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwepo kwa ubaguzi wa kimfumo nchini Uswisi hususan dhidi ya watu weusi wenye asili ya Afrika.

Ripoti hiyo imetegemea matokeo ya uchunguzi wa siku kumi wa tume ya kutafuta ukweli ya maafisa wa Umoja wa Mataifa. Mnamo Januari mwaka huu, wajumbe wa tume hiyo walisafiri katika mikoa tofauti ya Uswisi na kukutana na raia wenye asili ya Afrika, wanasiasa, wawakilishi wa polisi na wawakilishi wa mashirika ya kiraia nchini Uswisi.

Mwishoni mwa utafiti wao, ujumbe huo ulifikia hitimisho kwamba Uswisi ina tatizo lililojificha la chuki na ubaguzi wa rangi, hasa kuhusu watu wenye asili ya Afrika.

Ripoti hiyo imeashiria matukio mawili muhimu likiwemo la kesi ya Nzoy Roger Wilhelm ambaye alipigwa risasi na kuuliwa na polisi wakimshuku kuwa na kisu.

Imeelezwa katika ripoti ya Umoja wa Mataifa kwamba Nzoy Roger Wilhelm ni mhanga wa sera maalumu ya kuwafuatilia raia wa jamii za waliowachache kimbari na kirangi. Kesi ya pili inahusiana na Brian Kane, kijana mwenye umri wa miaka 26 na raia wa Uswisi ambaye amekuwa gerezani tangu 2018, ingawa madaktari wamegundua kuwa ana ugonjwa wa  nakisi ya umakini (ADHD).

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imesema kwamba kesi ya Brian ni mfano wa wazi wa ubaguzi wa rangi.

Waraka wenye vipengele 59 wa tume ya Umoja wa mataifa umeelezea matatizo mbalimbali yanayowakabili watu weusi nchini Uswisi, ikiwa ni pamoja na "ripoti za kutisha za ukatili wa polisi".

Ripoti hiyo ya UN pia imekosoa "utambuzi usiotosha" wa uhusiano wa Uswizi na ukoloni na biashara ya utumwa barani Afrika, ambayo inasema imechangia moja kwa moja katika utajiri wa sasa wa nchi hiyo, haswa kupitia faida ya benki na viwanda vilivyohusishwa na utumwa hapo awali.

Wataalamu wa Kikundi Kazi cha Umoja wa Mataifa kuhusu Waafrika, walioshiriki katika mkutano wa 51 wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa, wamelaani ubaguzi wa rangi dhidi ya raia wenye asili ya Afrika nchini Uswisi na kutangaza kuwa hali ya haki za binadamu ya raia hao inahitaji kushughulikiwa haraka.

342/