Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) ametoa ujumbe rasmi wa rambirambi kufuatia kifo cha Hujjatul-Islam wal-Muslimin Sheikh Ali Mayunga, mmoja wa Wanachuoni Mashuhuri wa Kiislamu Afrika Mashariki na Mwanachama wa Jumuiya hiyo nchini Tanzania.
Katika ujumbe huo uliosainiwa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s), Ayatollah Reza Ramezani, ameeleza kupokea kwa huzuni kubwa taarifa ya Kifo cha Marehemu, akieleza kuwa amekuwa mfano wa kujitolea katika kuhudumia Uislamu na Ahlul-Bayt (a.s).
Ujumbe huo umeeleza kuwa Sheikh Ali Juma Mayunga aliyatumia maisha yake katika kufufua na kuhuisha urithi halisi wa Kiislamu, kufanya uhakiki wa vitabu vya thamani, pamoja na kusambaza elimu na utamaduni wa Ahlul-Bayt (a.s) nchini Tanzania.
Aidha, Marehemu alikuwa na mchango mkubwa katika nyanja za kielimu, ikiwemo nafasi yake kama Katibu wa Baraza la Wanazuoni wa Ahlul-Bayt (a.s), na alikuwa miongoni mwa waliotafsiri Qur’an Tukufu kwa lugha ya Kiswahili iliyoitwa Tafsiri Al-Mubin.
Jumuiya hiyo kupitia Katibu Mkuu wake imetoa rambirambi kwa familia ya Marehemu, Ndugu, Jamaa na Wapenzi wake, pamoja na jamii ya Kiislamu kwa ujumla, na kumuomba Mwenyezi Mungu amshushie Marehemu Rehema Zake pana, amsamehe madhambi yake na amjaalie daraja ya juu Peponi.
Mwisho wa ujumbe huo, Karibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul-Bayt (a.s) amewaombea wafiwa subira, faraja na malipo mema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akisisitiza kuwa mchango wa marehemu katika elimu na da‘wah utaendelea kukumbukwa na kuenziwa.

Your Comment