Main Title

source : Parstoday
Jumanne

5 Machi 2024

18:57:45
1442457

Ghasia zashadidi Haiti, waziri mkuu hajulikani aliko baada ya safari yake Kenya

Majirani wa Haiti wameanza kuimarisha ulinzi wao na kuwarejesha nyumbani wafanyakazi wa balozi zao huku ghasia za magenge katika taifa hilo la Karibea zikiongezeka "kwa kiasi kikubwa," wakati ambao waziri mkuu wa nchi hiyo aliyekuwa safarini Kenya hajulikani yuko wapi.

Serikali ya Haiti Jumapili ilitangaza hali ya hatari ya saa 72 na kuweka marufuku ya kutotoka nje usiku baada ya magenge yenye silaha kuvamia magereza makubwa mawili ya nchi hiyo na kuwaachilia maelfu ya wafungwa mwishoni mwa juma.

Magenge sasa yanadhibiti asilimia 80 ya mji mkuu wa Port-au-Prince, na yanapigania kuuteka mji huo kikamilifu.

Takriban watu 15,000 wanakadiriwa kukimbia mji huo kufuatia ufyatulianaji risasi mkali ulioanza Ijumaa.

Jamhuri ya Dominika ambayo inashiriki kisiwa cha Hispaniola na Haiti ilisema Jumatatu waziri wake wa ulinzi alitembelea mpaka wa nchi hiyo kutathmini hali ya usalama kwenye mpaka huo na "utayari wa kijeshi wa kufanyika operesheni."

Wakati huo huo, nchi jirani ya Bahamas imewaita nyumbani wafanyakazi wa ubalozi wake, na kuwaacha maafisa  wawili tu wa ubalozi wanaohusika na usalama.

Mexico pia imewashauri raia wake kutosafiri Haiti na kuwataka wale ambao tayari wako nchini humo kuepuka kufanya safari zisizo za dharura na kuhifadhi majumbani maji, mafuta na vitu visivyoharibika.

Viongozi wa magenge wanamtaka Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry ajiuzulu, ambaye hajulikani aliko tangu aliposafiri Kenya ambapo akiwa ameandamana na Rais William Ruto wa nchi hiyo walishuhudia kutiwa saini mapatano ya kutumwa askari polisi wa Kenya watakaoongoza kikosi cha kimataifa cha kukabiliana na magenge nchini Haiti chini ya uungaji mkono wa Umoja wa Mataifa.

Ghasia za magenge zimeikumba Haiti kwa miaka mingi, lakini zimeongezeka zaidi tangu kuuawa Rais Jovenel Moise mnamo 2021.

Henry, ambaye aliingia madarakani baada ya kuuawa Moise, alikuwa ameahidi kuondoka madarakani mapema mwezi Februari, lakini baadaye akasema lazima kwanza usalama uimarishwe upya ili kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki unafanyika.

Kufuatia kuahirishwa kuondoka madarakani Henry, magenge hatari sasa yanakadiriwa kudhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu. Umoja wa Mataifa unakadiria mzozo huo ulisababisha vifo vya takriban watu 5,000 mwaka jana na kupelekea wengine 300,000 kuhama makazi yao huku kukiwa na uhaba wa chakula na huduma za matibabu.

Msemaji wa Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi alisema nchi tano zimeuarifu rasmi Umoja wa Mataifa kuhusu nia yao ya kuchangia maafisa katika kikosi cha kimataifa cha kurejesha usalama Haiti, ambacho Henry aliomba kitumwe katika nchi hiyo haraka mwaka 2022. Haiti ni kati ya nchi maskini zaidi duniani na maskini zaidi katika bara la Amerika.