Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Rais wa Chuo Kikuu cha Ulinzi wa Taifa na Utafiti wa Kijeshi cha Iraq, Luteni Jenerali wa Rubani Aqeel Mustafa Mahdi, amesema kuwa taifa la Iraq halitasahau kamwe misaada na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kauli hiyo aliitoa alipokuwa akitembelea Chuo cha Uongozi na Makao Makuu ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ambapo alisisitiza kuwa uhusiano kati ya mataifa haya mawili jirani na rafiki - Iran na Iraq - ni wa kihistoria, na katika miaka ya karibuni umeimarika kwa kiwango cha kuridhisha, huku akitumaini utaendelea kukua zaidi.
Amesema, “Tunafurahia sana kwamba maafisa wa Iraq wanasoma katika Chuo cha Uongozi na Makao Makuu ya Jeshi la Iran. Ingawa kuna uwezekano wa kusoma katika nchi nyingine, tunapendelea maafisa wetu wapate elimu yao hapa Iran, kwa kuwa tunajua wanapata mafunzo bora chini ya wakufunzi wenye kiwango cha juu cha kielimu na kitaaluma.”
Katika ziara hiyo, Luteni Jenerali Aqeel Mustafa Mahdi pamoja na ujumbe wa ngazi ya juu kutoka Iraq walitembelea madarasa ya mafunzo, kituo cha michezo ya kivita, kitivo cha vita, makumbusho ya kijeshi, maktaba na madarasa ya lugha ya Kiajemi ya chuo hicho.
Kwa upande wake, Kamanda wa Chuo cha Uongozi na Makao Makuu ya Jeshi la Iran, Amir Sartip Hussein Valivand Zamani, alisema kuwa uhusiano wa kijeshi kati ya Iran na Iraq umeanza vizuri na kuna hamu kubwa ya kuuendeleza. Aliongeza kuwa wako tayari kubadilishana walimu ikiwa ushirikiano huo utaimarika zaidi.
Amir Sartip Valivand Zamani aliongeza:
“Tunatarajia mataifa yetu mawili yaendelee kushirikiana kwa mafanikio katika kutimiza malengo yao makubwa ya pamoja. Uhusiano wa Iran na Iraq ni uhusiano usioweza kuvunjika.”
Aidha, Naibu wa Elimu na Taaluma ya Juu katika chuo hicho, Amir Sartip wa Pili Gholamreza Nasirpour, aliwasilisha historia ya chuo, maendeleo yake, taaluma zinazotolewa, na mafanikio ya kielimu na ya mafunzo ya kijeshi.
Vilevile, siku ya Jumamosi tarehe 26 Mehr 1404 (sawa na 18 Oktoba 2025), Luteni Jenerali Aqeel Mustafa Mahdi alifanya ziara nyingine katika Chuo Kikuu cha Juu cha Ulinzi wa Taifa cha Iran (DAA), ambapo alikaribishwa na Sardar Sartip Ismail Ahmadi-Moqaddam, rais wa chuo hicho.
Wajumbe wa ujumbe wa Iraq walipata fursa ya kutembelea vitivo vya ulinzi, usimamizi na masuala ya kimataifa, pamoja na kukagua sehemu za malazi na huduma zilizotengwa kwa wanafunzi wa kigeni wa chuo hicho.
Your Comment