Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (as) -ABNA- Tukio muhimu la uchangiaji damu lililowakutanisha Shia Development Organization kwa ushirikiano na JAI limefanyika kwa mafanikio makubwa katika Manispaa ya Bukoba, mkoani Kagera, likiwa na lengo la kuokoa maisha ya wagonjwa wanaokabiliwa na upungufu wa damu katika hospitali za mkoa huo.

Waandaaji wa tukio hilo wamesisitiza umuhimu wa jamii kujitolea na kuwajali wananchi wasiojiweza, hususan wale waliolazwa hospitalini na wanaohitajika kuongezewa damu ili kuendelea kuishi. Wamesema misingi ya Mafundisho ya Kiislamu kupitia watukufu wa Ahlul-Bayt (a.s) inasisitiza thamani ya utu, kusaidiana na kujitoa kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa jamii.

Wananchi kutoka makundi mbalimbali walijitokeza kwa wingi kuchangia damu, hatua iliyotajwa kuakisi moyo wa ubinadamu, mshikamano na uzalendo. Zoezi hilo limeelezwa kuwa msaada wenye thamani kubwa unaogusa maisha ya wagonjwa wanaopambana na upungufu wa damu, akiwemo mama wajawazito, watoto na waathirika wa ajali.
Taasisi hizo zimeahidi kuendeleza kampeni ya uchangiaji damu mara kwa mara ili kufanikisha juhudi za sekta ya afya na kuokoa maisha ya watu wengi zaidi.

Your Comment