Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekutana na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Andrew Lentz, Ikulu ya Chamwino, kujadili ushirikiano wa kimkakati kati ya Tanzania na Marekani. Mazungumzo yao yalilenga kuimarisha mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama, huku yakijikita zaidi katika miradi mikubwa ya uwekezaji ya LNG, Tembo Nickel na Mahenge Graphite.

Miradi ya LNG na Tembo Nickel imefikia hatua za mwisho kabla ya kusainiwa rasmi, wakati Mradi wa Mahenge Graphite ukiendelea kupanuliwa. Rais Samia alisisitiza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na washirika wanaoheshimu uhuru na maslahi ya taifa, huku akibainisha kuwa miradi hiyo italeta ajira, kuongeza uwekezaji na kuchochea ustawi wa kiuchumi.
Kwa upande wake, Balozi Lentz alieleza kuwa ushirikiano wa Tanzania na Marekani umejengwa katika misingi ya ustawi wa pamoja, si utegemezi wa misaada, na kupongeza juhudi za Tanzania chini ya falsafa ya 4R na Dira ya Maendeleo ya 2050. Takribani makampuni 400 ya Marekani yanafanya kazi nchini, jambo linaloonesha kuimarika kwa mazingira ya uwekezaji.

Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya Dola za Kimarekani bilioni 43, ikilenga kuongeza uzalishaji wa nishati, kukuza sekta ya madini, kuimarisha viwanda, kuongeza ajira na kuinua nafasi ya Tanzania katika soko la kimataifa.

Your Comment