Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA- Hadithi za maisha ya Bibi Fatima Zahraa (a.s) zimejaa mifano ya upekee wa imani, ujasiri na mapenzi ya dhati kwa Baba yake, Mtume Muhammad (s.a.w.w).
Miongoni mwa matukio yanayoangazia nafasi yake tukufu ni msimamo wake thabiti alipokuwa akimtetea Mtume katika kipindi ambacho Quraysh waliongeza uadui na vitimbi dhidi yake, hususan baada ya kufariki Abu Talib.
Katika tukio maarufu lililonukuliwa na vitabu vya historia na hadith, Bibi Fatima (a.s) alienda kwa uchungu mkubwa kuondoa matumbo ya ngamia yaliyowekwa na washirikina kichwani mwa Mtume (s.a.w.w) wakati akiwa katika sajda. Tukio hili linabaki kuwa ushahidi wa mapenzi yake ya kipekee na ulinzi usioyumba kwa Mtume wa Uislamu(s.a.w.w).

Ufafanuzi Zaidi
Wakati ambapo - baada ya kufariki Abu Talib - uadui wa Quraysh dhidi ya Mtume uliongezeka, Fatima (a.s) alikuwa akimtetea baba yake dhidi ya hila na mateso ya washirikina na wapumbavu wa Quraysh.
Siku moja, Mtume alipokuwa ameinamisha kichwa chake akifanya sajda mbele ya Ka‘aba, baadhi ya washirikina — ‘Amr ibn ‘Ās na ‘Uqbah na wengineo - walichukua matumbo ya ngamia na kuliweka juu ya kichwa chake. Hapo binti yake Fatima akaja akiwa analia, akalitoa juu ya kichwa cha baba yake na kulitupa kando.
“Wakati uadui wa Quraysh dhidi ya Mtume (s.a.w.w) ulipozidi, Fatima (s.a) alikuwa akimtetea kutokana na vitimbi na madhila ya washirikina na wapumbavu wa Quraysh. Basi siku moja… walileta matumbo ya ngamia - jazūr - wakayainua na kuyaweka juu ya kichwa cha Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) naye akiwa katika sajda katika uwanja wa Ka‘aba… Basi binti yake Fatima (s.a) akaja akiwa analia, akayakumbatia yale matumbo na kuyaondoa juu yake kisha akayatupilia mbali.”
[Ahqāq al-Haqq, Juz. 25: 289; Sharh Nahj al-Balāgha, Juz. 6: 282]
Your Comment