7 Desemba 2025 - 17:40
Mufti wa Tanzania Atoa Wito wa Kulinda Amani na Kuepuka Uchochezi wa Kidini na Maandamano Yanayopangwa Kufanyika 9 Disemba

"Tuepuke upepo mbaya unaosambazwa kwa chuki za kidini. Sisi Waislamu hatukatazwi kuishi kwa wema na wasiokuwa Waislamu. Maisha ya watu lazima yalindwe,” alisema Mufti.

Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt as -ABNA-| Dar es Salaam – Tanzania, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Sheikh Dkt. Abubakar Zubeir Bin Ally Wambwana, ametoa wito mzito kwa Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla, kuendelea kulinda amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa, huku akionya vikali dhidi ya uchochezi wa chuki za kidini.

Mufti amesema kuwa Uislamu unasisitiza kuishi kwa wema na haki pamoja na watu wa dini zote, akibainisha kuwa Waislamu wamefundishwa na Mwenyezi Mungu kuheshimu uhai wa kila binadamu bila kujali dini au itikadi yake.

Tuepuke upepo mbaya unaosambazwa kwa chuki za kidini. Sisi Waislamu hatukatazwi kuishi kwa wema na wasiokuwa Waislamu. Maisha ya watu lazima yalindwe,” alisema Mufti.

Aidha, amewataka watu wote wanaohamasisha vitendo vya kuvuruga amani, hususan maandamano yaliyopangwa kufanyika tarehe 9 au 25, kuacha mara moja, akisisitiza kuwa vitendo hivyo vinaweza kuhatarisha usalama wa taifa na maisha ya raia.

Mufti pia amewaomba viongozi wa dini zote waendelee kuwa mabalozi wa amani na watulivu katika kauli na matendo yao, huku wananchi kwa ujumla wakihimizwa kuepuka maneno na vitendo vya uchochezi vinavyoweza kuleta mifarakano katika jamii.

Nawasihi Waislamu kote nchini kutojihusisha na maandamano hayo, na waendelee kulinda taswira njema ya dini yetu kwa vitendo vya amani, subira na hekima,” alisisitiza.

Wito huu wa Mufti unakuja katika kipindi nyeti ambacho nchi inahitaji mshikamano wa kijamii, maelewano ya kidini na umoja wa kitaifa ili kudumisha amani na maendeleo ya taifa.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha