7 Desemba 2025 - 18:24
Mtazamo wa Mapambano ya Sheikh Ghazal Dhidi ya Serikali ya Kigaidi ya Al-Jolani: Kuanzia Kukabidhi Silaha hadi Mwito wa Mgomo wa Kitaifa

Baada ya mabadiliko ya hivi karibuni nchini Syria, Sheikh Ghazal Ghazal, Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Waalawi, amekuwa akitoa misimamo mbalimbali akidai kulindwa kwa haki za Mashia wa Syria. Katika siku za hivi karibuni, ametoa mwito wa mgomo wa kitaifa wa amani kama sehemu ya kupinga mauaji na dhulma zinazotekelezwa na serikali ya mpito ya Al-Jolani.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Jina la Sheikh Ghazal Ghazal lilijitokeza wazi baada ya kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad tarehe 8 Desemba, kama mmoja wa viongozi wakuu wa kidini wa dhehebu la Waalawi nchini Syria. Mwanzoni alichukua msimamo wa tahadhari dhidi ya serikali mpya ya Al-Jolani, lakini hasa baada ya matukio ya Machi 2025 katika pwani ya Syria, alibadili mwelekeo na kuchukua msimamo mkali wa upinzani kamili dhidi ya serikali hiyo.

Sheikh Ghazal ni Rais wa Baraza Kuu la Kiislamu la Waalawi ndani na nje ya Syria, chombo cha juu kabisa kinachowakilisha Waalawi katika masuala ya kidini na kijamii. Kwa sasa, amekuwa mmoja wa viongozi wa kiroho wanaotegemewa zaidi na jamii ya Waalawi kwa mwongozo wa kisiasa na kijamii.

Kutoka Ajenda ya Kukabidhi Silaha hadi Mwito wa Mgomo na Kuundwa kwa Kamati ya Kimataifa ya Uchunguzi

Baada ya kuanguka kwa utawala wa Assad, Sheikh Ghazal alisema katika mahojiano na Abdallah Al-Ghadawi yaliyorushwa YouTube kuwa kukabidhi silaha kwa Waalawi kulifanywa kwa maelekezo ya viongozi wao kwa ahadi ya kulindwa, na akathibitisha kuwa yeye binafsi hakubeba silaha. Alithibitisha pia kuwa baada ya kuanguka kwa utawala huo, kulifanyika mikutano kadhaa kati yake na viongozi wa serikali mpya ya Syria.

Hata hivyo, baadaye alibadili msimamo wake kutoka kukubali kwa masharti serikali mpya hadi kuwa mpinzani wake waziwazi. Alikataa kuitambua kamati ya uchunguzi ya serikali kuhusu matukio ya pwani ya Syria, na katika ujumbe wa video uliochapishwa Julai, alitoa mwito wa kuingiliwa na jumuiya ya kimataifa.

Katika video hiyo, aliitaja serikali ya Al-Jolani kuwa ni “shirika kamili la kigaidi linalofuata dini iliyopotoshwa inayohalalisha umwagaji damu”. Alisisitiza kuwa hapati uhalali wa kidini wala kisheria kwa kamati hiyo, iwe siku ya kuundwa kwake au baada ya kutoa matokeo yake.

Kuundwa kwa Baraza Kuu la Kiislamu la Waalawi – Februari 2025

Katika tamko la kuanzishwa kwa Baraza Kuu la Kiislamu la Waalawi la Syria na nje ya nchi lililotolewa Februari 2025, likaasomwa na Basil Ali Al-Khatib, mwanaharakati wa kisiasa kutoka Tartus, Sheikh Ghazal Ghazal aliteuliwa rasmi kuwa Rais wa baraza hilo.

Kwa mujibu wa tamko hilo, baraza hilo limeundwa kama mfumo jumuishi wa kuwakilisha jamii ya Waalawi na kueleza malengo yao katika kipindi hiki muhimu cha historia ya Syria.

Baraza hili lina sehemu mbili:

1. Baraza la Kidini

Linaongozwa na Mufti Sheikh Ghazal Ghazal, likiwa na masheikh 130:

  • 30 kutoka Tartus
  • 30 kutoka Latakia
  • 30 kutoka Homs
  • 30 kutoka Hama
  • 10 kutoka Damascus na vitongoji vyake

Baraza hili hushughulikia masuala ya kidini.

2. Baraza la Utendaji

Lina ofisi zifuatazo:

  • Ofisi ya Kisiasa
  • Ofisi ya Mahusiano ya Umma
  • Ofisi ya Habari
  • Ofisi ya Uchumi
  • Ofisi ya Misaada
  • Ofisi ya Kisheria
  • Ofisi ya Uratibu
  • Ofisi ya Maridhiano ya Kihistoria

Tamko Kali Dhidi ya Mauaji na Ubaguzi wa Kisekta

Katika miezi ya hivi karibuni, Sheikh Ghazal ametoa matamko kadhaa akilaani mauaji ya wanamgambo wa Al-Jolani dhidi ya raia wa Syria. Katika moja ya matamko yake kufuatia mashambulizi ya Homs – mji wenye wakazi wengi wa Kiwalawi – alisema:

“Syria imegeuzwa kuwa uwanja wa migogoro ya kidhehebu. Waalawi kamwe hawajawahi kuwa na tatizo na kuongozwa na Masunni, Wakurdi, Druze au makundi mengine.”

Aliongeza kuwa: “Jamii ya Waalawi ilikabidhi silaha zake kwa msingi wa kuhalali kwa serikali. Lakini baadaye tukajikuta tukiishi chini ya serikali ya kigaidi, ya kikafiri, ya kibaguzi na yenye kutaka madaraka kwa nguvu.”
Akaongeza kuwa serikali ya mpito “hutumia Masunni kama chombo cha kisiasa, na kila sauti ya kudai haki hukabiliwa kwa hotuba za chuki.”

Mwito wa Haki ya Kisiasa na Ulinzi wa Kimataifa

Sheikh Ghazal amesema kuwa:

  • Mauaji, uhamisho wa nguvu, mateka na kukamatwa kiholela bado vinaendelea
  • Maelfu ya watu wamepotea bila mashtaka wala kesi
  • Hatima ya waliotekwa nyara bado haijulikani

Akaeleza pia: “Tunahitaji ramani ya wazi ya kisiasa na ratiba ya haraka ya kuunda serikali ya mpito, chini ya usimamizi wa moja kwa moja wa Jumuiya ya Kimataifa na Umoja wa Mataifa, kwa misingi ya katiba ya haki, kisheria na yenye uwazi – si katiba ya kutulazimishwa.”

Akizihutubia jamii ya Waalawi alisema: “Hili ndilo lengo letu, na hatutaliacha kwa vitisho, hongo wala ukaidi.”

Mwito wa Mgomo wa Kitaifa wa Siku Tano

Katika siku za hivi karibuni, Sheikh Ghazal Ghazal alitangaza mgomo wa kitaifa wa siku tano kama hatua ya amani ya kupinga hali ya sasa. Mgomo huo unaendelea kuanzia tarehe 8 hadi 12 ya mwezi huu, ambapo waandamanaji watabaki majumbani mwao bila kutoka nje.

Katika maelezo yake alisema: “Tulitarajia siku ya kuanguka (kwa utawala wa zamani) iwe siku ya mwisho wa udikteta, lakini kilichoanguka ni mabaki ya taifa chini ya jina la ‘uhuru’.”

Aliongeza kuwa: “Watu wanatishwa, wanauawa, wanatekwa, wanachinjwa, wanachomwa moto, na sasa hata riziki zetu zinatishiwa kwa kufukuzwa kazi, kuhamishwa kwa nguvu, dhulma na hofu, ili suluba tushirikishwe kwenye sherehe zinazojengwa juu ya damu na maumivu yetu.”

Tahadhari ya Mwisho

Sheikh Ghazal amewahi pia kusema: “Hatutakubali kamwe dola ya Kiislamu ya kisiasa itakayochinja watu kwa msingi wa utambulisho wao.”
Katika mahojiano na mtandao wa Al-Mayadeen aliongeza: “Kila shambulio dhidi ya Waalawi halitapita bila majibu.”

Kwa kuzingatia ukali wa vitendo vya kibaguzi vya serikali ya Al-Jolani, wachambuzi wanasema kuwa harakati za hivi karibuni za Mashia wa Syria – kuanzia kuundwa kwa makundi ya upinzani hadi kauli za Sheikh Ghazal – zinaweza kuibua mabadiliko makubwa ya kisiasa na kiusalama nchini Syria, na pia kuwakabili kwa changamoto kubwa Wazayuni walioko kusini mwa Syria.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha