Shirika la habari la ISNA limeripoti kuwa, Nasser Kan'ani ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kuhusu jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa kizayuni wa Israel na hali inayouzonga utawala huo unaoongozwa na Benjamin Netanyahu kwamba: "Baada ya kupita miezi 11 ya vita vya pande zote, vya umwagaji damu na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza ambavyo vimeua shahidi Wapalestina zaidi ya elfu 41 sasa kunashuhudiwa kushika kasi hitilafu ambazo hazijawahi kushuhudiwa huko nyuma kati ya viongozi wa Kizayuni, huku baadhi ya maafisa wa kisiasa, kijeshi na kiusalama wakijiuzulu nyadhifa zao, na maandamano na migomo ya umma ikiongezeka katika taasisi za Kizayuni."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kusema kuwa: Ulimwengu mzima unashuhudia mivutano ikiongezeka katika jamii na uongozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kadiri kwamba, baadhi ya viongozi wa Kizayuni na weledi wa mambo wanazungumzia hatari na mchakato wa kusambaratika Israel.
Vyombo vya habari vya Kizayuni pia hivi karibuni viliashiria vita dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza na kuuawa wanajeshi na maafisa wa kijeshi wa Israel na kukiri kuwa, ahadi zilizotolewa na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa Israel miezi 11 iliyopita kuhusu kuibuka na ushindi katika vita na kuiangamiza harakati ya Hamas, ni hadaa tupu na matamshi ya upotoshaji.
342/