4 Septemba 2024 - 19:18
Walowezi wa Kizayuni wapiga muziki na kufanya ibada zao kwenye eneo la Msikiti wa Ibrahimi

Jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel limeruhusu maelfu ya walowezi haramu kufanya tamasha la muziki na ibada zao katika eneo la Msikiti wa Ibrahimi ulioko kwenye mji wa Al-Khalil, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan unaokaliwa kwa mabavu baada ya kuufunga Msikiti huo usitumiwe na Waislamu Wapalestina.

Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii imewaonyesha wanajeshi wa Israel wakiwaruhusu walowezi hao wa Kizayuni kuhamishia baadhi ya vyombo vya muziki ndani ya Msikiti huo.

Klipu hiyo ya video, ambayo inavyoonekana, ilichukuliwa na walowezi au mwanajeshi wa Israel, imewaonyesha pia wanajeshi wa Kizayuni wakisaidia kuingiza vifaa ndani ya mahala hapo patakatifu pa ibada.

Mkurugenzi wa Msikiti wa Ibrahimi Moataz Abu Sneineh amesema, walowezi wa Israel walifanya tamasha katika viwanja vya Msikiti wa Ibrahimi "katika ukiukaji wa wazi wa maeneo ya ibada na faragha ya Waislamu."Abu Sneineh ameliambia shirika la habari la Wafa: "matendo na ukiukaji huu unafanyika katika fremu ya kubadilishana majukumu na wakoloni, kwa sababu vikosi vamizi vimewaruhusu kuleta vyombo vya muziki na vipaza sauti kama sehemu ya kuweka udhibiti kamili wa Msikiti na mazingira yake, wakati ambapo Wapalestina hawaruhusiwi kuleta vifaa muhimu kwa ajili ya Msikiti kwa ajili ya matengenezo na ukarabati".

Kwa mujibu wa Wafa, Msikiti wa Ibrahimi ulifunguliwa kwa ajili ya waumini wa Kipalestina mapema Jumanne.

Waislamu wanaupa umuhimu mkubwa Msikiti wa Ibrahimi, kwa sababu wanaamini kuwa ulijengwa juu ya kaburi la Nabii Ibrahim AS.

Itakumbukwa kuwa kufuatia mauaji ya waumini 29 wa Kipalestina mwaka 1994 ndani ya msikiti huo yaliyofanywa na  Baruch Goldstein, mlowezi wa Kiyahudi mwenye misimamo ya kufurutu mpaka, mamlaka za utawala wa Kizayuni zililigawanya jengo la Msikiti wa Ibrahimi kati ya waumini wa Kiislamu na Wayahudi.

Mji wa Al-Khalil una wakazi Wapalestina 220,000 na walowezi haramu wa Kizayuni wapatao 500 tu. Walowezi hao wanaishi kwenye maeneo yaliyozungukwa na makazi ya Wapalestina yaliyowekewa ulinzi mkali na wanajeshi wa Israel.../



342/