Main Title

source : Pars Today
Jumanne

1 Oktoba 2019

06:50:15
979562

Operesheni ya 'Ushindi kutoka kwa Allah' pigo kubwa la Wayemen kwa utawala wa Saudia mkoani Najran

Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah nchini humo, sambamba na kutekeleza operesheni iliyopewa jina la 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu' katika mkoa wa Najran, limeusababishia utawala wa Aal-Saud maafa na hasara kubwa.

(ABNA24.com) Jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah nchini humo, sambamba na kutekeleza operesheni iliyopewa jina la 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu' katika mkoa wa Najran, limeusababishia utawala wa Aal-Saud maafa na hasara kubwa.

Operesheni ya 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu' ambayo ni operesheni kubwa zaidi ya Wayemen dhidi ya utawala wa Saudi Arabia, inaweza kuchunguzwa katika pande kadhaa. Nukta ya kwanza ni kwamba operesheni hiyo ni ya nchi kavu. Hii ni kusema kuwa tangu mwezi Agosti hadi tarehe 14 ya mwezi uliomalizika wa Septemba, yaani kwa kipindi cha siku 45, Wayemen wametekeleza tu operesheni kubwa za anga dhidi ya Saudia. Katika hali ambayo utawala wa Aal-Saud umejikita katika kudumisha usalama wa anga kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi ya anga ya jeshi la Yemen na kamati za raia wa nchi hiyo, mara hii umeshambuliwa kutokea nchi kavu. Operesheni ya nchi kavu ya jeshi la Yemen na harakati ya Answarullah imethibitisha wazi kwamba si tu kuwa nguvu na uwezo wake unakomea kwenye operesheni za anga tu, bali uwezo huo pia unajumuisha nchi kavu nao ni mkubwa zaidi. Moja ya uthibitisho wa hayo ni ukubwa wa hasara ambayo imeipata Saudi Arabia katika operesheni hiyo. Nukta ya pili ya operesheni hiyo, ni kiwango cha hasara ulichokipata utawala wa Aal-Saud ambacho kinajumuisha hasara za kibinadamu na zisizo za kibinadamu.

Hii ni kusema kuwa katika uwanja wa kibinaadamu, kama alivyosema Brigedia Yahya Saree, Msemaji wa Jeshi la Yemen, maelfu ya askari wa adui wamejisalimisha na mamia ya wengine ikiwemo idadi kubwa ya makamanda, maafisa wa jeshi na askari wa Saudi Arabia, wametekwa nyara. Kwa upande usio wa kibinaadamu, sambamba na kuzisambaratisha kikamilifu brigedi tatu za jeshi la Saudia, pia kiasi kikubwa cha silaha na zana za kijeshi yakiwemo mamia ya magari ya kijeshi na ya deraya ya adui, yametwaliwa ngawira na Wayemen. Ama nukta ya tatu inahusiana na uga wa kijografia wa operesheni hiyo. Hii ikiwa na maana kwamba operesheni hiyo imetekelezwa katika mkoa wa Najran ndani ya ardhi ya Saudia. Inafaa kuweka wazi kuwa, Najran, Aseer na Jazan, ni mikoa mitatu ya Yemen ambayo Saudia iliikodi katika muongo wa 1930, hata hivyo hapo baadaye mikoa hiyo iliunganishwa na sehemu ya jografia ya Saudia na kukaliwa kwa mabavu na utawala huo. Hivi sasa jeshi la Yemen limesonga mbele kwa mamia ya kilometa ndani ya mkoa wa Najran sambamba na kuudhibiti. Ukweli ni kwamba kwa kutekeleza operesheni hiyo, askari wa Yemen wametoa ujumbe kwa utawala wa Aal-Saud kwamba, iwapo Riyadh haitositisha vita vyake nchini Yemen, basi kuna uwezekano wa kukombolewa mikoa hiyo mitatu kutoka kwa Saudia na kuirejesha Yemen. Hii ndio hali iliyotarajiwa hasa baada ya kujiri mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Yemen kwenye taasisi za mafuta za Saudia katika maeneo ya Buqayq na Khurais. 

Nukta ya nne ni kwamba, operesheni ya 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu' inaonyesha kwamba Wayemen wana machaguo mengi dhidi ya utawala wa Aal-Saud, ambapo kila moja linapotumika, huwa linatoa pigo kubwa kwa Riyadh kuliko la kabla yake. Katika uwanja huo tarehe Mosi Agosti mwaka huu, jeshi la Yemen kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Answarullah lilitekeleza operesheni ya Dammam, ambayo ilikuwa ni operesheni kubwa ya makombora dhidi ya Saudia, huku tarehe 17 ya mwezi huo huo likitekeleza operesheni nyingine kwa kushambulia taasisi ya mafuta ya Saudia ya Shaybah umbali wa kilometa 10 kwenye mpaka na Imarati. Operesheni hiyo ya ndege zisizo na rubani ilikuwa kubwa zaidi kuwahi kufanywa na jeshi la Yemen dhidi ya adui kufikia kipindi hicho. Hali ikiwa hivyo, tarehe 14 Septemba jeshi la Yemen na harakati ya Answarullah zilitekeleza shambulizi lingine kwa kutumia ndege 10 zisizo na rubani kwenye taasisi za mafuta za Saudia ARAMCO na kupelekea asilimia 50 ya uzalishaji mafuta katika kiwanda hicho kusimama sambamba na kuisababishia hasara kubwa serikali ya Riyadh. Hata kama operesheni ya 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu' inatofautiana na operesheni ya ARAMCO katika uga wa utekelezaji wake, lakini kuhusu ukubwa wake, operesheni hiyo inazidi shambulizi la shirika la mafuta la ARAMCO. Hivyo inatazamiwa kuwa hatua ijayo ya Wayemen dhidi ya Saudia itakuwa kubwa zaidi kuliko hata ya operesheni ya 'Ushindi kutoka kwa Mwenyezi Mungu.' Nukta ya mwisho ni hii kwamba hatua zote za kijeshi za jeshi la Yemen na harakati ya wananchi ya Answarullah dhidi ya Saudi Arabia, zinaonyesha kwamba, katika mwaka wa tano wa vita vya muungano vamizi wa Saudia, Wayemen wanakusudia kushinda vita hivyo, kama alivyoahidi Abdul-Malik Badreddin al-Houthi, Kiongozi wa Answarullah mwanzoni mwa mwaka wa tano wa vita hivyo kwa kusema kuwa, mwaka wa tano wa hujuma za adui dhidi ya Yemen utakuwa ni mwaka wa ushindi kwa taifa la Yemen.



/129