4 Machi 2023 - 16:55
Unene kupindukia tishio kwa dunia, nusu ya walimwengu kuwa wanene mno 2035

Ripoti mpya kabisa zilizoripotiwa leo Ijumaa na vyombo vya habari zinaonesha kukwa, zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani watakuwa wanene kupita kiasi na uzito wa kupitiliza mipaka ifikapo 2035 kama hatua kubwa hazitochukuliwa.

Ripoti iliyotolewa na Taasisi ya Kukabiliana na Unene wa Kupindukia Duniani ya 2023 inatabiri kwamba asilimia 51 ya walimwengu yaani zaidi ya watu bilioni nne, watakuwa wanene na wenye uzito wa kuchupa mipaka katika kipindi cha miaka 12 ijayo. 

Ripoti hiyo imesema, viwango vya unene wa kupindukia vinaongezeka haraka sana miongoni mwa watoto na hasa katika nchi zenye kipato cha chini.

Louise Baur, mkuu Shirikisho la Watu Wanene Duniani amesema, watunga mkono sera na mkakati wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia hali kuwa mbaya zaidi.

Amesema: "Inatia wasiwasi hasa kuona viwango vya unene vikiongezeka kwa kasi zaidi miongoni mwa watoto na vijana, tena katika nchi zenye kipato cha chini." 

Ameongeza kuwa: "Serikali na watunga sera ulimwenguni kote wanahitaji kufanya yote wawezayo kuhakikisha wanadhibiti hali hiyo kwa njia za kiafya, kijamii na kiuchumi kwa kizazi kipya."

Ripoti hiyo imegundua kuwa unene wa kupindukia kwa watoto unaweza kuongezeka maradufu kutoka idadi ya mwaka 2020 na kufikia hadi wavulana milioni 208 na wasichana milioni 175 ifikapo 2035.

Kwa mujibu wa taarifa ya shirikisho hilo, gharama kwa jamii na kwa serikali ni kubwa kutokana na hali ya kiafya inayohusishwa na unene uliopitiliza. Zaidi ya dola trilioni 4 kila mwaka ifikapo mwaka 2035 yaani sawa na asilimia 3 ya pato la taifa (GDP).

Hata hivyo, shirikisho hilo limesema kuwa haliwalaumu watu binafsi, bali wanatoa mwito wa kuzingatiwa masuala ya kijamii, kimazingira na kibaolojia yanayohusika katika hali hiyo ya unene na uzito wa kuchupa mipaka.

342/