Trump, mwenye umri wa miaka 77 ni rais wa kwanza wa Marekani kuwahi kushtakiwa na kisha kupatikana na hatia ya makosa ya jinai.
Jopo la wajumbe wa mahakama moja jijini New York, Alhamisi lilimpata na hatia mtawala huyo wa zamani wa Marekani kwa mashtaka 34 ya kugushi hati zake za biashara.
Hukumu ya Trump imepangwa kutolewa Julai 11, kati kati ya kampeni yake ya kutaka kuitawala tena Marekani, siku chache tu kabla ya kuanza kwa Kongamano la Kitaifa la chama chake cha Republican hapo Julai 15.
Rais huyo wa zamani, ambaye amekanusha mashtaka hayo dhidi yake, anatazamiwa kuchuana vikali na mgombea wa chama cha Democratic Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba.
Trump anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka minne jela kwa kila kosa, ingawa waangalizi wa mahakama wanasema kuna uwezekano kwamba atapunguziwa adhabu.
Akizungumza nje ya mahakama Trump amesema: "Hii ilikuwa kesi iliyoibwa na ya kufedhehesha. Hukumu ya kweli itakuwa ile ya wananchi mnamo Novemba 5. Wananchi wanajua kilichotokea hapa."
342/