9 Mei 2025 - 15:45
Watu 5 Wauawa Katika Shambulio la Mizinga la Jeshi la India katika eneo la Kashmir

Watu 5 Wasio Wanajeshi, Wakiwemo Mtoto Mmoja, Wauawa Katika Shambulio la Mizinga la Jeshi la India Katika Eneo la Kashmir Linalodhibitiwa na Pakistan.

Kwa mujibu wa Ripoti kutoka Shirika la Habari la Kimataifa la Ahlul-Bayt (a.s) -ABNA- Kutokana na mashambulizi ya mizinga yaliyofanywa na Jeshi la India, watu watano wasio wanajeshi, wakiwemo mtoto mdogo wa kike, wamepoteza maisha katika eneo la Kashmir linalodhibitiwa na Pakistan.
Shambulio hili limetokea huku India ikiishutumu Pakistan kwa kufanya mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (Droni) katika maeneo ya mpaka wa magharibi, na imetangaza kuwa jeshi lake liko tayari kujibu hatua yoyote ya Islamabad.

Kwa mujibu wa takwimu mpya, kufikia sasa idadi ya vifo kutokana na mapigano ya hivi karibuni tangu siku ya Jumatano imefikia watu 37 waliouawa na takribani 60 kujeruhiwa.
Wakati mvutano kati ya India na Pakistan ukizidi kupamba moto, mwandishi wa Al Jazeera ameripoti kutokea kwa mapigano makali na kurushiana risasi kati ya pande hizo mbili katika maeneo ya mpaka wa Kashmir, kwa mujibu wa vyanzo vya eneo la Kashmir inayodhibitiwa na Pakistan.

Chanzo cha usalama kutoka mkoa wa Punjab, Pakistan, kimeripoti kuwa jeshi la Pakistan limeuangusha ndege sita za kijasusi za India (droni) katika eneo la Okara siku ya Ijumaa asubuhi. Kwa mujibu wa maelezo yao, jumla ya droni 77 za upelelezi kutoka India zimeharibiwa tangu kuanza kwa mapigano.

Kutokana na kuongezeka kwa hali ya taharuki, Serikali ya Pakistan imetangaza kufunga anga yake kwa safari zote za kiraia, na shule, vyuo na taasisi zote za elimu katika jimbo la Punjab zimesitisha shughuli hadi wiki ijayo.

Mapigano haya yalianza siku ya Jumatano, baada ya India kufanya mashambulizi katika maeneo ya Pakistan, yakiwemo misikiti kadhaa, ikidai kuwa yalikuwa vituo vya wanamgambo wa kigaidi. Mashambulizi haya yalifuatia mlipuko wa kigaidi ulioua watu wengi mwezi uliopita katika Kashmir inayodhibitiwa na India. Hata hivyo, Pakistan imekanusha kuhusika kwa namna yoyote katika mashambulizi hayo.

Kwa upande mwingine, jeshi la India limetangaza kwamba usiku uliopita vikosi vya Pakistan vilitumia droni na silaha kushambulia maeneo ya India katika mpaka wa magharibi. Vyombo vya habari vya India vimeripoti kuwa Wizara ya Ulinzi imeitisha kikao cha dharura, huku ikiibuka taarifa kwamba jeshi la majini la India limeanza operesheni za kulipiza kisasi dhidi ya Pakistan.

Katika mahojiano na Al Jazeera, Shazia Ilmi, msemaji wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) nchini India, alidai kuwa Pakistan ndiyo kichocheo cha migogoro katika ukanda huo, na akasisitiza kuwa India inashambulia tu maeneo ya wanamgambo, si raia.

Lakini kwa upande wa Pakistan, Atāullah Tārrar, Waziri wa Habari, ameyaita madai ya India kuwa hayana msingi wowote, akisema kuwa jeshi la Pakistan halijafanya mashambulizi yoyote dhidi ya ardhi ya India au Kashmir inayodhibitiwa na India. Aidha, aliongeza kuwa jeshi la Pakistan liko katika hali ya tahadhari kamili.

Pia, amepinga vikali uvumi kuwa Pakistan imevamia au kushambulia mahekalu ya dini ya Kisikh, akisisitiza kuwa Pakistan ina uhusiano mzuri na makundi ya kidini, hususan jamii ya Wasikh.

Tags

Your Comment

You are replying to: .
captcha