Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, wataalamu 30 na maripota maalumu wa Umoja wa Mataifa wametangaza kuwa, watengenezaji na wasambazaji silaha kwa utawala wa Israel wanapaswa kusimamisha uuzaji wa zana za kijeshi kwa utawala huo hata kama watapata leseni za kusafirisha silaha nje ya nchi.
Wataalamu hao wa Umoja wa Mataifa wameeleza kuwa, tangu Mahakama ya Kimataifa ya Haki ilipoiamuru Tel Aviv kusitisha mashambulizi ya kijeshi katika mji wa Rafah ulioko kusini mwa Ukanda wa Gaza, kiwango cha hatari kwa makampuni ya silaha kimeongezeka.
Wameongeza kuwa, kuendelea kuipatia silaha Israel kunaweza kutambuliwa kama uungaji mkono wa makusudi kwa mashambulizi yanayokiuka haki za binadamu za kimataifa na sheria za kimataifa za kibinadamu.
Juzi (Juni 19), katika ripoti yake iliyotathmini mashambulizi 6 ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza, ambayo yamesababisha hasara kubwa, Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa ilitangaza kuwa kuna uwezekano kwamba utawala huo umefanya ukiukaji mwingine wa sheria za vita.Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa pia ilitangaza kuwa, vikosi vya jeshi la utawala wa Kizayuni vimekuwa vikiendelea kukiuka kanuni za kimsingi za sheria za vita na havitofautishi kati ya raia na wapiganaji kwenye mashambulizi yao za kijeshi katika Ukanda wa Gaza na mji wa Rafah.
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza ilitangaza Alhamisi iliyopita kwamba tangu tarehe 7 Oktoba 2023, Wapalestina 37,431 wameuawa shahidi katika mashambulizi ya kikatili ya Israel, na watu wengine 85,653 wamejeruhiwa katika Ukanda wa Gaza.
342/