Taarifa ya maafisa hao 12 wa Marekani waliojiuzulu wakipinga vita vya Gaza imeongeza kuwa, uungaji mkono na himaya ya pande zote ya Marekani kwa Israel na silaha inazotoa nchi hiyo kwa utawala huo ni kushiriki katika mauaji na kuwasababishia njaa watu wa Gaza. Maafisa wa Marekani waliojiuzulu wameeleza kuwa sera mbovu na zilizo kinyume na mantiki kuhusu Gaza ni tishio kwa Marekani na zinahatarisha pia maisha ya wanajeshi na wanadiplomasia wa nchi hiyo. Taarifa hiyo imesisitiza kuwa, sera za serikali ya Biden kuhusu Gaza zimedhoofisha nafasi na hadhi ya Marekani mbele ya walimwengu. Mwishoni mwa taarifa yao maafisa hao 12 wa Marekani waliojiuzulu nyadhifa zao wakilalamikia vita vinavyoendelea Ukanda wa Gaza kwa mara nyingine tena wamesisitiza kuwa sera ya sasa ya Marekani huko Ukanda wa Gaza itaendelea kuwadhuru Wapalestina, Waisraili na usalama wa taifa wa Marekani.
Taarifa ya maafisa 12 wa Marekani waliojiuzulu inaonyesha upendeleo na himaya ya pande zote ya Marekani mkabala wa vita na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina. Washington imekuwa na nafasi muhimu katika uvamizi wa utawala huo katika Ukanda wa Gaza kwa kuutumia maelfu ya mabomu huku ikitambua vyema jinai na mauaji ya kimbari yanayotekelezwa na utawala huo wa Kizayuni dhidi ya raia madhulumu wa Palestina. Pamoja na hayo lakini inaendelea kukanusha kuhusika moja kwa moja serikali ya Biden katika kuwauwa shahidi maelfu ya watu wa Gaza, khususan watoto na wanawake.
Bila shaka Marekani inapasa kutambuliwa kama mshirika wa moja kwa moja wa Israel katika jinai zake za kutisha dhidi ya Wapalestina huko Ukanda wa Gaza, kutokana na himaya na uungaji mkono wake wa pande zote wa kisiasa, kidiplomasia, kijeshi na kiusalama kwa Tel Aviv, na pia kukandamiza maandamano ya kupinga vita vya Gaza na kuwaunga mkono Wapalestina yanayoshuhudiwa ndani ya Marekani. Licha ya uungaji mkono mkubwa wa kisiasa na kijeshi wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni, na pamoja na utawala wa Kizayuni kupuuza matwaka ya jamii ya kimataifa likiwemo ombi la kutoshambuliwa mji wa Rafah, lakini serikali ya Biden na maafisa wa ngazi za juu wa Marekani hawatumii wenzo wowote wa mashinikizo ya kisiasa na kifedha ili kuilazimisha Israel isimamishe vita katika Ukanda wa Gaza zaidi ya kutoa maonyo ya maneno matupu kwa Tel Aviv. Ni wazi kuwa vita vya Gaza ni ishara ya kushindwa kimaadili sera za nje za Biden. Biden takriban amedhihirisha uungaji mkono wake kamili kwa utawala wa Kizayuni na viongozi wa utawala huo tangu kuanza vita dhidi ya Gaza. Serikali yake imetuma mamia ya shehena za silaha ambazo zimeliwezesha jeshi la Kizayuni kuendeleza vita vya kikatili huko Gaza. Si haya tu, bali Biden pia ametumia haki ya kura ya turufu ya Marekani katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuzuia maazimio kadhaa yaliyotaka kusitishwa vita katika Ukanda wa Gaza; na hata kudhoofisha itibari na uhalali wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) na Mahakama ya KImataifa ya Jinai (ICC) ambazo zimekuwa zikikosoa mauaji ya imati na jinai nyingine za Tel Aviv dhidi ya Wapalestina. Nukta muhimu ni kuwa ukingiaji kifua wa serikali ya Biden kwa utawala wa Kizayuni umekabiliwa pia na radiamali na upinzani mkubwa ndani ya taasisi tawala za Marekani. Kuhusiana na suala hilo, baadhi ya wafanyakazi wa serikali ya Marekani hasa ndani ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya nchi hiyo wamejiuzulu wakipinga vita vya Gaza na kulalamikia himaya ya serikali ya Biden kwa utawala wa Kizayuni. Huko nyuma wafanyakazi 100 wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Marekani walimwandikia barua Rais wa nchi hiyo wakimtuhumu kwa kuchapisha taarifa za upotoshaji kuhusu vita vya Gaza. Walieleza kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel umefanya jinai za kivita katika vita vya Gaza. Aidha zaidi ya wafanyakazi 130 wa Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani waliiandikia barua serikali wakitaka ichukue hatua za kusimamisha vita huko Gaza haraka iwezekanavyo. Mnamo Novemba 2023, zaidi ya wafanyakazi 700 wa taaisi na wizara zaidi ya 30 za Marekani walimwandikia barua Rais Joe Biden wa nchi hiyo, wakimwomba aunge mkono suala la kusimamisha vita huko Gaza.