25 Desemba 2024 - 16:43
Waislamu, Wakristo wana nukta nyingi za pamoja zaidi ya wanavyofikiri

IQNA - Wakati Krismasi ikiwa imewadia, afisa wa kundi kubwa zaidi la kutetea Waislamu nchini Marekani, akinukuu aya za Qur’ani Tukufu, amengazia jinsi Waislamu wanavyomheshimu Yesu au Nabii Isa (AS).

Katika makala yake, Ibrahim Hooper, Mkurugenzi wa Kitaifa wa Mawasiliano wa Baraza la Mahusiano ya Kiislamu na Marekani (CAIR) lenye makao yake makuu mjini Washington, amesisitiza kwamba Waislamu na Wakristo wana mambo mengi zaidi yanayofanana zaidi ya wanavyofikiri.

Ifuatayo ni makala yake:

“Na pale Malaika walipo sema: Ewe Maryamu! Hakika Mwenyezi Mungu anakubashiria (mwana) kwa neno litokalo kwake. Jina lake ni Masihi Isa mwana wa Maryamu, mwenye hishima katika dunia na Akhera, na miongoni mwa walio karibishwa (kwa Mwenyezi Mungu).”

Kabla ya kutafuta nukuu hii katika Agano Jipya, unaweza kwanza kumuuliza mfanyakazi mwenzako Mwislamu, rafiki au jirani yako nakala ya Qur’ani, maandishi ya Uislamu yaliyoteremka kutoka kwa Mwenyezi Mungu.  Nukuu hii imetoka katika Aya ya 45 ya sura ya 3 ndani ya Quran.

Inajulikana sana, hasa katika msimu huu wa sikukuu, kwamba Wakristo hufuata yale wanayoamini kuwa mafundisho ya Yesu. Kinachoeleweka vyema ni kwamba Waislamu pia wanampenda na kumheshimu Yesu ambaye wanamuita Nabii Isa (Amani ya Mwenyezi Mungu Iwe Juu Yake-AS-) kama mmoja wa wajumbe wakuu wa Mungu kwa wanadamu.

Aya nyingine katika Qur’anI, zinazochukuliwa na Waislamu kuwa neno la moja kwa moja la Mungu, zinasema kwamba Yesu aliimarishwa na “Roho Mtakatifu” (2:87) na ni “ishara kwa ulimwengu wote.” (21:91) Kuzaliwa kwake na bikira kulithibitishwa wakati Maryamu ananukuliwa akiuliza: “Nitapataje mwana na hali hakuna mtu aliyewahi kunigusa?” (3:47)

Qur’ani Tukufu  inamwonyesha Nabii Isa (AS) akizungumza kutoka kwenye utoto na, kwa idhini ya Mwenyezi Mungu, akiwaponya wakoma na vipofu. (5:110) Mwenyezi Mungu pia anasema katika Qur’anI: “Tena tukafuatisha nyuma yao Mitume wengine, na tukamfuatisha Isa bin Mariamu, na tukampa Injili. Na tukajaalia katika nyoyo za walio mfuata upole na rehema.” ( 57:27 )

Wakati nguvu za chuki katika nchi hii na ulimwenguni pote zinavyojaribu kuwatenganisha Waislamu na Wakristo, tunahitaji sana nguvu ya kuunganisha ambayo inaweza kuziba pengo linaloongezeka la kutokuelewana na kutoaminiana kati ya dini mbalimbali. Nguvu hiyo inaweza kuwa ujumbe wa upendo, amani na msamaha uliofundishwa na Yesu na kukubaliwa na wafuasi wa imani zote mbili.

Wakristo na Waislamu wangefanya vyema kuzingatia aya nyingine katika Quran inayothibitisha tena ujumbe wa Mungu wa milele wa umoja wa kiroho: “Semeni nyinyi: Tumemuamini Mwenyezi Mungu na yale tuliyo teremshiwa sisi, na yaliyo teremshwa kwa Ibrahim na Ismail na Is-hak na Yaakub na wajukuu zake, na waliyo pewa Musa na Isa, na pia waliyo pewa Manabii wengine kutoka kwa Mola wao Mlezi; hatutafautishi baina ya yeyote katika hao, na sisi tumesilimu kwake..” (2:136)

Mtume Muhammad (SAW) mwenyewe alitaka kufuta tofauti zozote kati ya ujumbe aliofundisha na ule uliofundishwa na Yesu, ambaye aliita “roho na neno la Mungu.” Mtume Muhammad (SAW) amesema: “Mimi ni mtu wa karibu kuliko watu wote duniani na Akhera kwa Isa bin Maryamu. Manabii ni ndugu wa baba; mama zao ni tofauti, lakini dini yao ni moja.

Waislamu wanapomtaja Mtume Muhammad, daima huongeza maneno “amani iwe juu yake na familia yake.” Wakristo wanaweza kushangazwa kujua kwamba maneno kama hayo huwa yanafuatana na Mwislamu kutaja Yesu au kwamba tunaamini kwamba Yesu atarudi duniani katika siku za mwisho kabla ya hukumu ya mwisho. Kutomheshimu Yesu, kama ambavyo tumeona mara nyingi sana katika jamii yetu, ni jambo la kuudhi sana kwa Waislamu.

Kwa bahati mbaya, matukio ya vurugu na matamshi yaliyojaa chuki kote ulimwenguni hutoa fursa ya kutosha ya kukuza uadui wa kidini. Na ndio, Waislamu na Wakristo wana mitazamo tofauti juu ya maisha na mafundisho ya Yesu. Lakini urithi wake wa kiroho unatoa fursa mbadala kwa watu wa imani kutambua urithi wao wa pamoja wa kidini.

Jumuiya ya Waislamu wa Marekani iko tayari kuheshimu urithi huo kwa kujenga madaraja ya maelewano ya dini mbalimbali na kutoa changamoto kwa wale ambao wangegawanya taifa letu kwa misingi ya kidini au kikabila.

Tuna mengi ya yanayofanana kuliko tunavyofikiri.

iqna