20 Februari 2025 - 19:56
Kwa nini Iran inakaribisha kuimarisha na kupanua uhusiano na nchi jirani?

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hivi karibuni amekutana na kuzungumza na Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan, Waziri Mkuu wa Tajikistan na Naibu Mkuu wa Baraza la Mawaziri la Turkmenistan. Mazungumzo haya yamefanyika pambizoni mwa Mkutano wa Tatu wa Kiuchumi wa Eneo la Kaspi hapa mjini Tehran.

Katika mazungumzo Jumanne wiki hii na Alexey Overchuk Naibu Waziri Mkuu wa Russia ambaye alifanya safari hapa nchini kwa shabaha ya kushiriki katika MKutano wa Tatu wa Kiuchumi wa Eneo la Kaspi, Rais Masoud Pezeshkian alisema kuwa kusainiwa mkataba wa makubaliano ya pamoja ya kistratejia kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Shirikisho la Russia ni moja ya madhihirisho muhimu ya ushirikiano kati ya nchi mbili na akasema: 'Viongozi wa nchi mbili wanapasa kutoa kipaumbele katika ajenda yao ya kazi kwa suala la utekelezaji wa mkataba huu.'

Katika mazungumo hayo na Naibu Waziri Mkuu wa Russia, Rais wa Iran ametathmini mchakato wa ushirikiano baina ya nchi mbili katika uga wa nishati, sekta ya viwanda, uchukuzi na biashara kuwa mzuri sana na chanya na kusema: 'Taasisi za kikanda na kimataifa zikiwemo taasisi za Eurasia, BRICS na Shanghai pia zimefungua majukwaa mapya ya ushirikiano wa pamoja, na wanatumai kuwa kwa kustafidi na fursa hizo, watu wa nchi mbili yaani Iran na Russia watanufaika na manufaa yake haraka iwezekanavyo.'

Naibu Waziri Mkuu wa Russia pia ameema katika mazungumzo hayo kuwa: 'Tumefurahishwa sana na kutiwa saini makubaliano ya kina ya ushirikiano wa kistratijia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, maingiliano na ushirikiano kati ya nchi hizi mbili umekuwa na nguvu zaidi baada ya kutiwa saini makubaliano haya, na kuongezeka kwa mabadilishno ya jumbe za kidiplomasia kati ya pande mbili ni kiashirio muhimu katika uwanja huu.'

Rais Pezeshkian aidha alikutana na kuzungumza na Ali Asadov Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan ambaye alifanya ziara mjini Tehran kwa lengo la kushiriki katika Mkutano wa Tatu wa Kiuchumi wa Eneo la Kaspi na kusema: "Mipaka ya kisiasa haiwezi kuwa kizuizi katika uhusiano na mfungamano mkubwa kati ya nchi na mataifa haya mawili."

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Azerbaijan pia ameashiria kiwango kizuri sana cha uhusiano kati ya nchi mbili na kusema: 'Serikali ya Azerbaijan imeazimia kuendeleza uhusiano wa pande zote na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran; na tuko tayari kuunga mkono na kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya nchi mbili.'Mazungumzo na mashauriano kati ya Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Tehran na viongozi wa nchi nne jirani yanaashiria kuendelea azma ya serikali ya 14 ya kuzidisha maelewano na ushirikiano katika nyuga mbalimbali, mwelekeo chanya wa ustawi wa nchi jirani na mikakati yao kwa ajili ya kuendeleza uhusiano wa pande zote.

Hatua na misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa kigezo chema cha kuzidisha ushirikiano na nchi jirani; na nchi nyingi za eneo hili hii leo zinafuata mkondo huo wa kidplomasia uliofanikiwa.

Wakati huo huo suhula na uwezo mkubwa wa kiuchumi wa nchi zinazopakana na Bahari ya Kaspi ni sababu chanya na athirifu kwa ajili ya kuendeleza ushirikiano huu tajwa, uwekezaji wa pamoja na wa nchi mbili na uimarishaji mikataba ya kikanda ili kukabiliana na ushawishi wa nchi ajinabi. 

Vile vile historia mbaya ya Marekani na Magharibi kwa lengo la kuzusha mvutano katika eneo imezifanya nchi zinazopakana na Bahari ya Kaspi kuimarisha uhusiano wa pande mbili na wa pamoja.

Iran, ikiwa ni nchi yenye uwezo na suhula mbalimbali za kiuchumi, kisiasa, kiutamaduni na kijamii na rasilimali watu imara na yenye uwezo itakuwa na mchango chanya katika kuathiri vyema mshikamano na ushirikiano mkubwa na nchi jirani.

Hatua ya Rais Pezeshkian ya kutilia mkazo mazungumzo ya pande mbili na viongozi wa nchi za Russia, Azerbaijan, Turkmenistan na Tajikistan kuhusu ushirikiano wa kiutamaduni, kisiasa na kiuchumi na kuimarisha uhusiano, ni sehemu ya hatua na malengo yajayo ya Iran kwa ajili ya mustakbali wa eneo. 

Sisitizo la Iran la kuimarisha ushirikiano na taasisi za kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na kuimarisha uhusiano na taasisi za Euroasia, BRICS na Shanghai pia itaibua majukwaa mapya ya ushirikiano wa pamoja na nchi jirani.



342/