Mazoezi haya yaliyoanza Jumatatu Machi 10 na kuzinduliwa rasmi Jumanne, yanahusisha vikosi vya majini vya Iran, Russia na China, pamoja na waangalizi kutoka nchi za Jamhuri ya Azerbaijan, Afrika Kusini, Oman, Kazakhstan, Pakistan, Qatar, Iraq, Umoja wa Falme za Kiarabu, na Sri Lanka. Meli za Jeshi la Majini la Iran na Kikosi cha Majini cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) pia zinashiriki katika mazoezi haya.
Lengo kuu la mazoezi haya ni kuboresha usalama wa majini na ushirikiano endelevu wa safari za baharini katika eneo la Kaskazini mwa Bahari ya Hindi. Aidha, mazoezi haya yanalenga kuonyesha uwezo wa vikosi vya majini vya Iran kimataifa, kuimarisha uwezo wao wa kitaalamu katika mafunzo ya kijeshi ya pamoja na kuendeleza diplomasia ya baharini ya Iran.
Mwishoni mwa mwaka jana, Iran, China na Russia pia zilifanya mazoezi mengine ya pamoja ya usalama wa majini (Ukanda wa Usalama wa Baharini 2024) katika eneo hilo hilo.
Vikosi vya majini vya Iran, China na Russia vinashiriki mazoezi haya kwa malengo tofauti, lakini muungano wao wa kimkakati unatoa ujumbe muhimu kwa mataifa ya eneo na dunia. Ushirikiano huu unaonyesha kiwango cha juu cha ushirikiano wa kijeshi kati ya mataifa haya matatu, ambayo mara nyingi hunashirikiana katika masuala ya kimataifa.
Kupitia mazoezi haya, mataifa haya yanapanua uratibu wa operesheni za majini na kuonyesha uwezo wao wa kufanya kazi kwa pamoja dhidi ya vitisho vinavyoweza kutokea.
Mazoezi haya pia yanaweza kufasiriwa kama jibu kwa mashinikizo ya kisiasa na kijeshi kutoka Magharibi, ikiwa ni pamoja na vikwazo dhidi ya Iran na Russia au uwepo wa kijeshi wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Hindi. Kufanyika kwa mazoezi haya karibu na njia muhimu za kimkakati kama vile Lango Bahari la Hormuz ni ujumbe wa wazi kwa mataifa ya Magharibi kuwa Iran, China, na Russia ziko tayari kulinda maslahi yao.
Kanda ya Kaskazini mwa Bahari ya Hindi, Bahari ya Oman, na Ghuba ya Uajemi ni miongoni mwa njia muhimu zaidi za biashara duniani, hasa kwa usafirishaji wa mafuta na gesi. Takribani asilimia 20 ya mafuta ya dunia hupitia Lango Bahari la Hormuz. Mazoezi haya yanaonyesha ahadi ya mataifa haya matatu katika kulinda usalama wa baharini na kukabiliana na vitisho kama uharamia na ugaidi wa baharini. Pia yanadhihirisha azma yao ya kuhakikisha usalama wa kanda bila kutegemea miungano ya Magharibi.
Kikosi cha Majini cha Iran kimefanya zaidi ya doria 100 katika bahari za kimataifa, zikiwemo Bahari ya Hindi, Bahari ya Pasifiki, Bahari ya Mediterania, Bahari Nyekundu na Ghuba ya Aden, hata kufika kilomita 3,000 karibu na Ghuba ya Meksiko, kwa ajili ya kupambana na uharamia na ugaidi.
Jeshi la Majini la Iran linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio katika kulinda Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, likiimarisha uwepo wake wa kimataifa kupitia operesheni mbalimbali za kijeshi, na kuonyesha uwezo wake kwa mataifa yenye nia ya kuhatarisha usalama wa bahari na bahari kuu.
Mazoezi haya pia yanatoa ujumbe kwa mataifa ya kigeni ambayo yanachangia ukosefu wa usalama katika eneo, yakionyesha azma ya mataifa ya kanda, hususan Iran, katika kulinda maslahi yao na kuhakikisha uthabiti wa eneo.
Lengo kuu la mazoezi haya ni kufanikisha malengo ya usalama, kisiasa na kijeshi, huku vikosi vya majini vya mataifa yanayoshiriki vikionyesha uwezo wao mkubwa wa kuyatekeleza.
Mazoezi ya pamoja ya Ukanda wa Usalama 2025 yanaonyesha kuwa nguvu halisi katika maji ya kimataifa si Marekani au mataifa ya Magharibi, bali ni mataifa huru ambayo yanafanya juhudi za kufanikisha malengo yao bila kutegemea ulimwengu wa Magharibi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Jeshi la Majini la Iran limeendelea kupeleka vikosi vyake katika bahari mbalimbali za kimataifa, likionyesha uwezo wake mkubwa wa kulinda usalama wa baharini. Pia, limepiga hatua kubwa katika utengenezaji wa vifaa vya kijeshi vya kisasa, likifanikiwa pakubwa katika maendeleo ya teknolojia ya kivita.
342/
Your Comment