Amir Saeid Iravani alisema hayo jana Ijumaa katika kikao cha ngazi ya juu cha Umoja wa Mataifa cha kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Chuki dhidi ya Uislamu na kueleza kuwa "Utawala wa Kizayuni" unatumia chuki dhidi ya Uislamu kama chombo cha kuhalalisha ukaliaji wake (wa mabavu wa ardhi ya Palestina) na jinai dhidi ya Wapalestina.
Akigusia uvamizi wa utawala wa Kizayuni na kuendelea kuwakandamiza wananchi wa Palestina, mwanadiplomasia huyo mwandamizi wa Iran katika UN amesisitiza kuwa, kila siku walimwengu wanashuhudia hujuma za kinyama dhidi ya Wapalestina wanaonyongeshwa katika ardhi yao.
Amesema, "Utawala unaoghusubu (ardhi ya Palestina) kwa kushirikiana na washirika wake, unajaribu kuhalalisha uhalifu wake wa kivita, sera za ubaguzi wa rangi, na ukandamizaji wa kimfumo kwa kuibua uhusiano bandia kati ya Uislamu na ugaidi."
Amesisitiza kuwa, Ummah wa Kiislamu unakabiliwa na vurugu, kukashifiwa, na kuvunjiwa heshima maadili, haram na kitabu chao kitakatifu katika nchi mbali mbali za Magharibi chini ya kivuli cha uhuru wa kujieleza.
Hapo jana, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alisema kuna "ongezeko la kutatanisha la chuki dhidi ya Uislamu" kote ulimwenguni huku akizitaka majukwaa ya teknolojia ya mtandaoni kuzuia matamshi ya chuki na unyanyasaji.
Guterres alisema hayo kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Uenezaji Chuki Dhidi ya Uislamu (Islamophobia) ambayo huadhimishwa kila tarehe 15 ya mwezi Machi na akatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuonyesha mshikamano.
342/
Your Comment