Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Kimataifa la Ahl al-Bayt (AS) -Abna-; Sima Bahous, Mkurugenzi Mtendaji wa Idara ya Umoja wa Mataifa ya Wanawake, akizungumzia kuendelea kwa marufuku ya elimu ya wasichana wa Afghanistan, amesema kuwa wasichana wa nchi hii wanapaswa kurejea shuleni haraka iwezekanavyo.
Jumatatu usiku (Machi 24, 2025), Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa alichapisha ujumbe kwenye jukwaa la X na kusema kuwa katika hali ya sasa, haki za kimsingi za Wanawake na Wasichana wa Afghanistan zinapaswa kurejeshwa.
Kulingana na Bi Bahous, na mwanzo wa mwaka mpya wa masomo nchini Afghanistan, milango ya shule na vyuo vikuu bado imefungwa kwa maelfu ya wasichana kwa mwaka wa tatu mfululizo.
Aliongeza kuwa kunyimwa elimu ni ukiukaji wa haki za watoto wa kike kupata elimu na kutadhuru vizazi nchini Afghanistan.
Wakati huo huo, Stephen Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa pia ameelezea wasiwasi wake kwamba ikiwa sera hii ya serikali ya Taliban itaendelea, takriban wasichana milioni nne wa Afghanistan watakuwa wamenyimwa elimu ifikapo mwaka 2030.
Katika mkutano na wanahabari siku ya Jumatatu, msemaji wa shirika hili, huku akiwaomba Taliban kufungua tena shule, alielezea matumaini kwamba marufuku ya elimu ya wasichana haitaendelea kwa miaka mitano zaidi.
Inafaa kuashiria kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) liliripoti kuwa zaidi ya wasichana 400,000 walikosa elimu katika mwaka mpya wa shule (au wa kimasomo).
Shirika hili la Umoja wa Mataifa lilikuwa limetoa takwimu hapo awali kwamba kwa sasa idadi ya wasichana walionyimwa elimu imefikia milioni 2.2.
Your Comment