30 Machi 2025 - 17:29
Source: Parstoday
Araqchi: Mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Yemen yanadhihirisha namna nchi hiyo inavyoshiriki katika uvunjaji wa sheria wa Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amelaani mashambulizi ya kijeshi ya mara kwa mara ya Marekani katika maeneo mbalimbali ya Yemen na kusema: Mashambulizi ya kijeshi ya Marekani huko Yemen sambamba na kushtadi mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na hujuma zake dhidi ya Lebanon na Syria, yanaonyesha namna Marekani inavyoshiriki katika uvunjaji sheria wa Israel na kwenda sambamba na utawala huo katika kueneza machafuko na hali ya mchafukoge katika eneo.

Sayyid Abbas Araqchi ameeleza masikitiko yake kuhusu ufahamu usio sahihi wa Marekani mkabala wa watu wa Yemen na wa kanda hii na kusisitiza kuwa: Wanasiasa wa Marekani wanapaswa kuelewa kwamba, chanzo kikuu cha ukosefu wa usalama katika eneo hili ni kuendelea hatua za mabavu na mauaji ya kimbari huko  Palestina inayokaliwa kwa mabavu, na kwamba Marekani haiwezi kudai kurejesha uthabiti katika eneo kwa kuishambulia Yemen na kuwaua watu wasio na hatia wa nchi hiyo ambao kosa lao pekee ni kudhihirisha mshikamano na kuwaunga mkono wananchi wanaodhulumiwa wa Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameeleza haya katika mazungumzo na "Hans Grundberg", Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Yemen, ambaye alifanya ziara hapa Tehran kwa ajili ya mazungumzo na mashauriano na viongozi wa Iran.

Mkuu huyo wa  chombo cha diplomasia wa Iran amekosoa kutochukua hatua Baraza la Usalama la UN mkabala wa ukiukaji wa wazi wa hati na sheria za kimataifa unaofanywa na utawala wa Israel na Marekani na kusisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaopasa kuchukua hatua chanya haraka iwezekanavyo ili kusitisha uvunjaji na ukiukaji wa sheria unaofanywa na Marekani na Israel.  

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha