30 Machi 2025 - 17:35
Source: Parstoday
Kuongezeka hatua za Trump dhidi ya vyuo vikuu na wanafunzi wanaowatetea Wapalestina

Katika muhula wake wa pili wa urais, Donald Trump, rais mpya wa Marekani kwa mara nyingine tena ameamua kutumia mtindo alioutumia katika muhula wake wa kwanza wa kuuunga mkono bila mpaka utawala wa Kizayuni wa Israel na kuchukua hatua mpya za kuisaidia na kuihami Israel dhidi ya Wapalestina.

Hatua hizi ni pamoja na kukandamiza wanafunzi wa vyuo vikuu na watetezi wa Wapalestina ndani ya Marekani.

Baada ya Trump kukata msaada kwa Chuo Kikuu cha Columbia mjini New York kutokana na mgomo na maandamano ya wanafunzi wake dhidi ya Wazayuni, chuo hicho kimelazimika kuchukua hatua za kumridhisha bwana mkubwa! Katika mondo huo, David J Greenwald, mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu cha Columbia, ametangaza katika taarifa kwamba Katrina Armstrong, rais wa muda wa chuo kikuu, amejiuzulu na kurejea katika nafasi yake ya awali na kuongoza kituo cha matibabu cha chuo hicho. Kujiuzulu kwa Armstrong kunakuja wakati wa msukosuko mkubwa ndani ya chuo hicho.

Wiki iliyopita pia, Chuo Kikuu cha Columbia kilikubali kutekeleza msururu wa mabadiliko makubwa ili kupata msaada wa dola milioni 400 kutoka kwa serikali ya Marekani. Serikali ya Trump inadai kuwa chuo hicho hakijafanya vya kutosha kukabiliana na eti chuki dhidi ya Wayahudi na kupinga maandamano ya watetezi wa Gaza. Mabadiliko hayo ni pamoja na kuundwa kikosi kipya cha polisi cha Chuo Kikuu cha Columbia, marufuku ya matumizi ya barakoa na kuondolewa udhibiti wa jopo la wanasayansi katika Idara ya Mashariki ya Kati, Asia Kusini na Afrika.

Wanachama wa Chuo Kikuu cha Columbia, pamoja na wengine, wamekosoa sana hatua hiyo wakiitaja kuwa ni kusalimu amri kusiko na mfano kwa ushawishi wa kigeni. Mbali na tishio la kupunguzwa kwa ufadhili, Chuo Kikuu cha Columbia pia kimekumbwa na ukandamizaji mkubwa dhidi ya wanaharakati wa wanafunzi wa kigeni ambao walitangaza uungaji mkono wao kwa watu wa Gaza wakati wa maandamano yaliyofanyika kwenye chuo hicho 2023 na 2024 pindi Israel ilipokuwa ikitekeleza mauaji ya kimbari huko Palestina. 

Katika mkondo huo, polisi wa uhamiaji wamemkamata Mahmoud Khalil, mhitimu na mwanaharakati wa wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Columbia, kwa sababu tu ya kueleleza maoni yake ya kuwatetea Wapalestina. Serikali ya Marekani inataka kumfukuza Khalil ambaye ana kadi ya kijani (green card), lakini amefungua kesi, akisisitiza kuwa ameadhibiwa kwa kutumia haki yake ya uhuru wa kusema na kujieleza, ambayo inalindwa na Katiba ya Marekani. Siku chache zilizopita Khalil aliandika ujumbe uliosambaa katika mitandao ya kijamii akijitaja kuwa ni mfungwa wa kisiasa nchini Marekani. "Jina langu ni Mahmoud Khalil, na mimi ni mfungwa wa kisiasa," amesema Khalil katika barua iliyochapishwa Jumanne iliyopita. "Kukamatwa kwangu ni matokeo ya moja kwa moja ya kutumia haki yangu ya uhuru wa kujieleza, kwa sababu nimetetea 'Palestine Huru' na kutaka kukomesha mauaji ya kimbari huko Gaza, ambayo yalianza tena kwa nguvu Jumatatu usiku," aliongeza katika barua hiyo, akimaanisha mashambulizi mapya ya anga ya Israel huko Gaza ambayo mamlaka za eneo hilo zinasema yameua zaidi ya Wapalestina 400.

Kuongezeka hatua za Trump dhidi ya vyuo vikuu na wanafunzi wanaowatetea Wapalestina

Kukamatwa Mmarekani huyo mwenye asili ya Palestina mnamo Machi 8 kulizua maandamano katika miji mbalimbali ya Marekani, ikiwa ni pamoja yale ya jiji la New York Jumanne, wakati mamia walipokusanyika Times Square wakitaka aachiliwe huru.

Trump anadai kuwa "waandamanaji hao wana chuki dhidi ya Wayahudi na wanaunga mkono wanamgambo wa Hamas."

Kinyume chake, watetezi wa Palestina, yakiwemo baadhi ya makundi ya Kiyahudi, wanasema wakosoaji wao wanachanganya kimakosa baina ya ukosoaji wa mashambulizi ya Israel dhidi ya watu wa Gaza na chuki dhidi ya Wayahudi, na uungaji mkono wao kwa haki za Wapalestina na eti kuunga mkono wanamgambo wa Hamas.

Wakati huo huo, zaidi ya wabunge 100 wa chama cha Democratic wamehoji uhalali wa kuwekwa kizuizini Mahmoud Khalil katika barua iliyotumwa kwa utawala wa Trump.

Shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa, kesi ya Khalil inawakilisha mtihani kwa mahakama za Marekani kuhusu jinsi ya kuainisha uhuru wa kujieleza unaodhaminiwa kwa raia chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani.

Mashambulio ya utawala wa Kizayuni dhidi ya Ukanda wa Gaza na mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko Palestina viliibua wimbi kubwa la maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Marekani na katika nchi nyingine kadhaa za Magharibi.

Kuongezeka hatua za Trump dhidi ya vyuo vikuu na wanafunzi wanaowatetea Wapalestina

Maandamano ya wanafunzi nchini Marekani kuunga mkono Palestina yanaweza kutambuliwa kuwa ni tukio jipya katika mfumo wa kisiasa na kijamii wa nchi hiyo. Ukandamizaji mkali dhidi ya wanafunzi wa vyuo vikuu, mashirika ya wanafunzi na maprofesa wa vyuo vikuu wanaoikosoa Israel nchini Marekani kwa sababu tu ya kuwatetea watu wa Palestina, kwa mara nyingine tena umefichua uongo wa kauli mbiu na madai ya nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusu haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

342/

Your Comment

You are replying to: .
captcha