Nchi kadhaa za Waislamu kama vile Saudi Arabia, Qatar, Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati), Bahrain, na Kuwait, zinasherehekea sikukuu ya Idul-Fitri leo Jumapili.
Duru za habari zinaarifu kuwa, baadhi ya Waislamu wameswali na kuadhimisha sikukuu ya Iddi hii leo katika nchi ya Kenya huku wengine wakitazamiwa kuswali kesho. Akthari ya Watanzania wanatazamiwa kuadhimisha siku hii tukufu kesho Jumatatu.
Hapa nchini Iran, Swala ya Iddul-Fitri inatazamiwa kuswaliwa kesho Jumatatu katika Musalla ya Imam Khomeini hapa Tehran. Swala hiyo itaswalishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, hapa mjini Tehran.
Indonesia, nchi yenye Waislamu wengi zaidi duniani, pamoja na Pakistan, Malaysia, Brunei, India, Jordan, Syria, Oman, Bangladesh, na Australia, pia zimetangaza Jumatatu kuwa siku ya kwanza ya Iddi.
Matangazo sawa na hayo yametolewa nchini Misri, Morocco, Tunisia na Libya ambapo mamlaka za kidini zilithibitisha kuwa leo Jumapili itakuwa siku ya mwisho ya Ramadhani.
Sherehe za Idi hutanguliwa na Swala ya Idul Fitri kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kukamilisha ibada adhimu ya funga ambayo ni nguzo muhimu katika dini ya Kiislamu. Iddi husherehekewa kwa siku tatu katika nchi zenye Waislamu wengi. Hata hivyo, idadi ya siku za mapumziko kwa ajili ya sherehe hizo inatofautiana nchi kwa nchi.
Redio Tehran inatoa mkono wa kheri, baraka na fanaka kwa Waislamu kote duniani kwa mnasaba wa sikukuu hii adhimu ya Waislamu.
342/
Your Comment